EACC yaanika ushahidi dhidi ya Obado na familia
TUME ya Maadili na Kukabili na Ufisadi Nchini (EACC) jana ilianika wazi jinsi familia ya aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado, mkewe, wanawe na watu wa ukoo wake walivyoshiriki katika unyakuzi wa mali ya kaunti kujitajirisha.
Akitoa ushahidi katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani Nairobi, afisa wa EACC Robert Ronoh alifichua jinsi alipata hati za ununuzi wa majumba ya kifahari katika vyumba vya kulala vya Obado na mwanawe Dan Achola.
Bw Ronoh alisema hati hizo zilikuwa zimefichwa katika majumba hayo mjini Migori na Loresho Nairobi.
“Maafisa wa EACC walivamia makazi ya Obado Migori na Nairobi na kupata hati za umiliki wa majumba kifahari,” alidokeza Bw Ronoh alipoanza kutoa ushahidi dhidi ya kesi inayomkabili Obado, Achola, Susan Scarlet Akoth, Jerry Zachary Okoth na Evelyne Zachary.
Wengine walioshtakiwa ni shemejiye Carolyne Anyango Ochola, Joram Opala , Patroba Ochanda na mama yao Peninah Auma.
Mahakama ilielezwa kuwa mkewe Obado Christine Akinyi Ochola, alikuwa na ardhi ya ekari moja na nusu.
Kesi inaendelea.
Ripoti ya Richard Munguti, Jael Maunda na Mumbi Wainaina