Habari za Kitaifa

Maalim aitwa na NCIC kwa madai ya kutishia ‘kuchinja’ Gen-Z waliovamia Bunge

Na CHARLES WASONGA July 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Daadab Farah Maalim sasa amejipata kikaangoni kwa kudaiwa kunaswa kwenye video akisema angewaangamiza vijana wa Gen Z waliovamia majengo ya bunge mnamo Juni 25, 2024.

Tume ya Uwiano wa Kitaifa na Utangamano (NCIC) sasa imemwagiza kufika mbele yake Julai 11, 2024 ili adadisiwe kuhusiana na madai hayo ya uchochezi.

Nacho chama cha Wiper, kilichomdhamini bungeni, kimejitenga na matamshi ya Bw Maalim ambaye alihudumu kama Naibu Spika wa Bunge la Kitaifa kati ya 2008 hadi 2013.

Kwenye taarifa Jumatano Julai 10, 2024, tume hiyo inayoongozwa na Kasisi Samuel Kobia ilisema imeanzisha uchunguzi kuhusiana na kauli ya mbunge huyo kwamba “ningekuwa rais ningeamuru kuchinjwa kwa Gen-Zs wote waliotekeleza kitendo cha uhaini kwa kuvamia majengo ya bunge Juni 25, 2024.”

“Maagizo hayo yametolewa kwa mujibu wa Sehemu ya 27 ya Sheria ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano Nambari 12 ya 2008, inayosema kuwa NCIC ina mamlaka ya kuwaita na kuwachunguza mashahidi na watu wengi wanaoshukiwa kutoa matamshi yanayofasiriwa kuchochea chuki, uhasama, au vita,” NCIC inasema kwenye taarifa.

Aidha, Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la Wiper chini ya uongozi wa Kalonzo Musyoka limependekeza kuwa Bw Maalim apokonywe majukumu yake bungeni na kiti chake cha ubunge “endapo itabainika kuwa alitoa vitisho kama hivyo.”

“Aidha, Maalim atavuliwa wadhifa wa Naibu Kiongozi wa Wiper,” chama hicho kikasema kwenye taarifa.

Mbunge huyo wa Daadab pia ni Mwanachama wa Jopo la Spika katika Bunge la Kitaifa na huhudumu kama Spika wa Muda endapo Spika Moses Wetang’ula au Naibu wake Gladys Boss Shollei hawapo.

Bw Maalim ameagizwa kufika mbele ya NCIC saa chache baada ya kupuuzilia mbali kanda iliyozungushwa mitandaoni ikisheheni madai yake.

“Kanda hivyo imevurugwa kwa kupachikwa maneno hapa na pale. Kimsingi inatoa madai ya uwongo na yasiyo na maana yoyote,” Bw Maalim akanukuliwa akisema.

Hii ni baada yake kurushiwa cheche za shutuma na Wakenya mitandaoni, haswa vijana waliopendekeza kwamba akamatwe na kushtakiwa.