• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
KINYUA BIN KING’ORI: NCIC ikomeshe wanasiasa ambao tayari wameanza kueneza chuki, uchochezi

KINYUA BIN KING’ORI: NCIC ikomeshe wanasiasa ambao tayari wameanza kueneza chuki, uchochezi

Na KINYUA BIN KINGORI

WANASIASA wengi hasa wagombeaji wa wadhifa wa Urais nchini hawana sera za kuaminika licha kuanza kampeni zao mapema.

Ni kwa sababu hiyo baadhi yao huishia kutumia kiwango kikubwa cha fedha kuwahonga wafuasi wao kuzuia wapinzani wao kuelezea sera kwa wapigakura .

tabia hii inafaa kukomeshwa 2022 na wananchi wazalendo kwa kuamua kuchukua jukumu la kuwapiga msasa wawaniaji wote kabla ya kuwachagua kushikilia nyadhifa za uongozi.

Japo Tume huru ya uchaguzi na Mipaka (IEBC) haijatangaza rasmi muda wa kampeni ,inashangaza na hata kuvunja moyo kuona baadhi ya wanasiasa wakijipiga vidari kutishia wapinzani na hata kuwaonya dhidi ya kuandaa mikutano ya kisiasa katika maeneo fulani nchini wakisingizia ni ngome zao.

Je, wanasiasa hao wanafahamu kujaribu kuzuia wenzao kuandaa mikutano katika eneo fulani ni sawa na kuchochea chuki kisiasa?.

Ni haki ya kikatiba ya kila mwananchi kuandaa au kuhudhuria mikutano ya kisiasa katika maeneo yoyote nchini bila kutishiwa na yeyote serikali ikiwemo.

Hisia zangu zangu leo zimevutiwa na matamshi ya Seneta wa Kakamega Cleophas Malala ambaye ni mwandani wa kinara wa chama cha ANC Musalia Mudavadi kwa kutishia kuvuruga mkutano wa Azimio la Umoja, ukanda wa magharibi unaotarajiwa kufanyika kesho Ijumaa katika uwanja wa Bukhungu kwa madai eti Mudavadi na Wetangula hawajaalikwa katika hafla hiyo.

Kinara wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) Samuel Kobia anafaa kujitokeza waziwazi kukabili wanasiasa ambao wameanza kutishia uhai wa Usalama na amani kwa kuanza kutoa matamshi ya kuchochea yanayoweza kuzaa chuki na kuvuruga Umoja na utaifa wetu.

Viongozi kama malala wanafaa kuchukuliwa hatua za kisheria mapema bila huruma au upendeleo ili iwe funzo kwa wengine wenye sifa potovu kueneza chuki kisiasa na kikabila.

Siasa haiwi sababu ya kueneza uhasama nchini, kundi la Raila kuandaa mikutano magharibi haiwi sababu ya kina malala kuwatia kiraka demkorasia kwa kueneza migawanyiko kisiasa au kikabila.

Tunaweza kutofautiana kisiasa na tuwe tunashabikia vyama mbalimbali lakini tusikiuke uhuru wa demkorasia yetu,wala kuhatarisha amani nchini.

Haina maana kwa tume ya Mzee Kobia kumwalika Malala katika Ofisi zao kumhoji kufafanua kiini cha matamshi yake na kumwacha huru bila kuadhibiwa.

Mtindo huu wa Tume ya NCIC umekuwa sawa na kuchezea shere umma na hulka ya wanasiasa kuzingatia chuki kisiasa itaendelea kutukuzwa hasa katika uchaguzi mkuu ujao wa 2022.

Kiongozi yeyote ambaye anaonekana kufurahia utundu wa kutimiza matakwa yake kwa kutishia wapinzani na kuchochea chuki kwa wananchi hafai kusamehewa bila kuchukuliwa hatua kali kwa maana anatishia ufaafu wa demkorasia na usalama nchini.

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: Watu kupotezwa: Serikali ithibitishe kuwa...

Utangulizi wa uchambuzi wa hadithi ‘Tulipokutana Tena’

T L