Makala

Mama apewa talaka kwa kuruhusu mabinti kucheza kandanda

Na FRIDAH OKACHI July 11th, 2024 2 min read

NDOA za wanawake kadhaa zimesambaratika baada ya kuidhinisha mabinti wao kucheza mpira wa kandanda kinyume na tamaduni za jamii yao katika Kaunti ya Wajir.

Asilimia kubwa ya wasichana kati ya miaka saba na 17 wanazuiwa kushiriki michezo inayochukuliwa kuwa ya wanaume pekee.

Bi Halima Yussuf amelazimika kuishi na rafikiye wa karibu baada ya kupewa talaka kwa kuidhinisha mabinti wake wawili kujiunga timu ya Malkia wa Wajir.

Alieleza Taifa Leo Dijitali kwamba mapema mwaka 2024, aliondoka kwenye ndoa kwa kukosa kuelewana na mumewe sababu ya kuidhinisha mabinti wake walio na vipaji vya kucheza mpira wa miguu.

Kulingana naye, sababu ya kuruhusu wanawe kucheza mpira ni kunoa makali ya vipaji vyao pamoja na kupata karo.

“Wanangu wana vipaji vya kucheza. Kuwazuia kucheza haikuwa haki. Lakini baba yao alipoamua niondoke, tuliondoka na wao,” alisema Bi Yussuf.

“Mume wangu alisema kuwaruhusu kucheza ni kinyume na tamaduni zetu. Kuna wenyeji wa huku wako Nairobi na wanacheza mpira. Mbona niwazuie kufanya wanachopenda?” Aliuliza Bi Yussuf.

Kilichomvutia zaidi ni baada ya wanawe hao kushiriki shindano la kwanza la Talanta Hela na kutuzwa kwa fedha ambazo ziliwezesha mmoja wao kujiunga na shule ya upili ya kutwa.

“Ilikuwa ni mara ya kwanza kutoka kwenye mji wetu kwao kushiriki shindano, kila mmoja alirejea na pesa. Hizo pesa zikatumika kulipa karo. Hata hivyo mume wangu hakuona faida yeyote,” alifichua Bi Yussuf.

“Kuna mmoja ambaye hakuwa amejiunga na shule na alipata pesa za kulipa karo,” alieleza Bi Yussuf.

Akiwa mwingi wa matumaini, Bi Yussuf ana matamanio ya wanawe kuwa wachezaji wa timu ya kitaifa baada ya kukamilisha masomo yao. Pia, aliwataka wazazi wenza kuwaruhusu watoto kukuza vipaji vyao kando na masomo.

“Inaumiza kupewa talaka. Sasa nimebaki kuwa mama na baba kwa sababu mzee hataki kuhusika nasi. Ombi langu ni kuona wakiimarika siku zijazo,” alisononeka.

Michezo mbalimbali pia inatumika kuwazuia vijana kujihusisha na mambo yasiofaa. Mama huyo wa watoto saba alisema wakati wa wikendi wasichana hao hutumia muda mwingi kucheza.

“Michezo huepusha mimba za mapema miongoni mwa wasichana. Sasa hivi hawana sababu ya kutoka nyumbani na kuzurura ovyo.”

Baadhi ya wasichana wanaocheza mpira katika kaunti hiyo, wengi hulazimika kucheza wakiwa na hijabu. Sheria na tamaduni za jamii hii zikieleza kuwa nywele ya binti haifai kuonekana.