Wakazi wa Eldoret wapongeza Ruto kwa kufuta mawaziri, wamuonya dhidi ya kuteua wanasiasa
BAADHI ya wakazi wa Uasin Gishu mjini Eldoret wamempongeza Rais William Ruto kwa kuvunja baraza la mawaziri huku wakimuonya dhidi ya kuwateua wanasiasa katika baraza lake lijalo.
Wakizungumza mjini Eldoret mnamo Alhamisi mara baada ya tangazo la Rais Ruto, walitaja hatua hiyo kama mwamko mpya wa ujasiri.
Wakiongozwa na mmoja wa wanaharakati wa Gen Z, Sharon Lagat, walisema wajumbe wengi wa baraza la mawaziri ambao wamepoteza kazi ni watu waliojawa na kiburi.
“Ninamsifu Rais Ruto kwa hatua hiyo lakini ninamwonya dhidi ya kuwateua tena katika baraza lake kwani wengi wao walikuwa wamejaa kiburi,” alisema Bi Lagat.
Bi Lagat alimwambia rais ateue tu mawaziri walio na ujuzi katika wizara.
Alisema mawaziri wengi wa baraza la mawaziri kutoka jamii ya Wakalenjin wamemezwa na kiburi.
“Ninamwambia Rais Ruto asimteue tena mwana wetu Murkomen. Ni miongoni mwa mawaziri ambao wamemfeli. Mara tu Murkomen alipojiunga na baraza la mawaziri, alimezwa na kiburi. Asiteuliwe tena,” Bi Lagat asema.
Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri North Rift CIPK Sheikh Abubakar Bini alimtaka Rais Ruto kukoma kuwateua wanasiasa katika nyadhifa za baraza la mawaziri.
“Tumepokea tangazo la kuvunja baraza la mawaziri kwa furaha kubwa, tumekuwa tukisubiri tangazo hili kubwa. Ninamtahadharisha dhidi ya kuteua watu bila ujuzi katika wizara yoyote,” alisema Sheikh Bini.
Alimtaka rais kuteua wataalamu katika baraza la mawaziri atakalobuni baadaye.