Habari za Kitaifa

Wamumbi: Gachagua aliniita mwaka jana na kunitaka nimsaliti Ruto


MBUNGE wa Mathira Eric Wamumbi amedai kuwa tofauti za kisiasa kati yake na Naibu Rais Rigathi Gachagua zilianza mwaka jana, Naibu Rais alipomtaka kuondoka katika serikali ya Rais William Ruto.

Bw Wamumbi alidai kuwa badala yake Bw Gachagua alimtaka ajishughulishe na mikakati ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Kwa muda sasa kumekuwa na vita vya maneno kati ya wawili hao, Naibu Rais akidai kuwa Bw Wamumbi anatumiwa wa watu fulani serikalini kumhujumu kisiasa.

Tofauti kati ya wawili hao zilifikia kilele Jumapili, Bw Gachagua alipodai mbunge huyo anatumiwa na maafisa wengine katika Wizara ya Usalama kuhujumu kampeni yake (Naibu Rais) ya kupambana na pombe haramu katika eneo la Mlima Kenya.

Bw Gachagua alisema hayo alipokuwa akihutubu katika ibada ya Jumapili katika kanisa moja kijijini Kiamariga, eneo bunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri.

Wawili hao wamekuwa wandani wa kisiasa, kiasi kwamba ni Bw Gachagua alimfanyia kampeni Bw Wamumbi katika uchaguzi mkuu wa 2022 hadi akashinda.

“Sina tofauti zozote za kibinafsi na Naibu Rais na ninamheshimu kwa sababu alinisaidia sana. Lakini kama mwanadamu unaweza kutofautiana hata na babako mzazi lakini unafanya hivyo kwa heshima,” Bw Wamumbi akasema.

Akaongeza: “Mwaka jana aliniita na kuniambia kwamba wakati umejiri kwa sisi kuondoka Kenya Kwanza na kuanza kampeni za kuelekea 2027. Lakini nikajiuliza mbona tuondoke katika serikali ambako tuna idadi kubwa ya mawaziri, kwa hakika 10, akiwemo naibu rais.”

Bw Wamumbi alisema hakuelewa mantiki ya ushauri wa Bw Gachagua kwa sababu maslahi yao yamelindwa katika serikali ya sasa inayoongozwa na Rais Ruto.

“Nilitofautiana naye alipopendekeza kuwa tuanze kampeni ilhali watu wetu wanashikilia nyadhifa kuu serikalini na wanaweza kusaidia watu wetu,” akaeleza.

Ufichuzi wa hivi punde wa Bw Wamumbi, unashadidi tofauti zinazoendelea kushuhudiwa ndani ya serikali ya Kenya Kwanza.

Haya yanajiri wakati ambapo tofauti kati ya Rais Ruto na Bw Gachagua zimejitokeza waziwazi huku ikidaiwa kuwa umaarufu wa wawili hao umeanza kudorora katika eneo la Mlima Kenya.