Habari za Kitaifa

Corona inavyosambaa watu wakidhania ni mafua – Utafiti


WATAALAMU wa afya wameonya kuhusu ongezeko la visa vya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, usio hatari, mwezi huu, Julai, hadi Agosti 2024.

Kulingana na Mshirikishi wa Mipango wa Kamati ya Ushauri kuhusu Covid-19 katika Muungano wa Kiuchumi wa Eneo la Ziwa (LREB) Profesa Shem Otoi Odhiambo, watu wamekuwa wakishindwa kutofautisha kati ya mafua ya kawaida na Covid-19.

“Dalili za Covid-19 na mafua ni karibu sawa. Kutokana na hali hiyo wagonjwa hawapewi matibabu yanayofaa. Siku hizi hospitali nyingi hazifanyi vipimo vya Covid-19,” akasema Prof Otoi.

Akaongeza: “Watu wanaelekeza juhudi zao katika mambo mengine. Wagonjwa wenye dalili za Covid-19 hawapimwi na hawapewi dawa ambazo zitapunguza kiwango cha virusi vya Covid-19 au Mafua.”

Prof Otoi alisema kuwa kulingana na uchunguzi wao, zaidi ya watu 200,000 wameambukizwa ugonjwa wa Covid-19 lakini usiohatarisha maisha.

“Kulingana na ukadiriaji wetu, karibu watu 40 wamelazwa hospitalini wakiugua Covid-19 na wanahitaji kuwekewa mitambo ya kuwaongezea hewa ya Oksijeni,” akasema.

Mtaaalamu huyo alieleza kuwa watu wenye magonjwa mengine kama vile Kisukari wako katika hatari ya hali yao kuwa mbaya endapo wataambukizwa virusi vya Covid-19.

Vile vile, alisema Covid-19 inaweza kuhatarisha maisha ya watu ambao kinga za miili yao ni dhaifu, wale wasiopata chanjo pamoja na wakongwe.

“Covid-19 ilikuwa hatari zaidi wakati wa kuchipuza kwa aina virusi kama vile Delta, Alpha, Omega na Omicron. Mtu aliyeambukizwa Covid-19 isiyo kali hapaswi kuongezewe Oksjeni au kulazwa hospitalini,” Prof Otoi akaeleza.

Wagonjwa kama hao wanaweza kusaidia kupata nafuu kutokana na matibabu mazuri ya nyumbani.

Kenya ilithibitisha kuwa mwenyeji wa Homa ya Corona mwaka wa 2020, na miaka miwili baadaye ulimwengu ukathibitishwa kuwa huru.

Mataifa mengi, raia walipewa chanjo dhidi ya ugonjwa huo hatari unaosababishwa na virusi vya corona.

Janga hilo la kimataifa liliharibu na kusambaratisha mikondo ya kawaida ya maisha, kufuatia kanuni na amri zilizowekwa kusaidia kudhibiti kuenea zaidi kwa Covid-19.