Maandamano: Ukarimu wa Mkahawa wa Java kwa Gen Z
HUKU maandamano ya Gen Z kupinga sera ‘dhalimu’ za serikali yakishika kasi maeneo tofauti nchini, Kaunti ya Nairobi imeshuhudia mchezo wa paka na panya kati ya vijana na maafisa wa polisi.
Maandamano hayo ya Jumanne, Julai 16, 2024 yanaendelezwa miji mikuu, wanaoshiriki wakitaka serikali ya Rais William Ruto kuangazia gharama ya juu ya maisha.
Maafisa wa usalama, licha ya Kaimu Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi, IG, Douglas Kanja kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuruhusu maandamano ya amani, polisi wanaoshika doria wameonekana kuchangia mambo kuwa mabaya zaidi kwa kurushia raia gesi ya vitoa machozi.
Hayo yakiendelea, Mkahawa wa Java katika barabara ya Kimathi, Jijini Nairobi umeonyesha ukarimu wa kipekee kwa waandamanaji.
Java ni tajika kwa huduma za uuzaji kahawa moto, dawa – mchanganyiko wa limau (ndimu), tangawizi na asali, ikiwa ni pamoja na vitafunio.
Mkahawa huo ulikuwa torokeo na mwokozi wa vijana walipofurushwa na polisi waliokabiliana nao.
Nje ya mkahawa huo, Gen Z walikuwa wakiamba ngoma ya mara kwa mara, kukosoa serikali ya Kenya Kwanza.
Katika kisa cha kuridhisha, ulikuwa huru kuruhusu vijana walioandamana kwa amani kuingia ndani vitoza machozi viliporushwa.
Gesi yenye mwasho ikitawala majukwaa ya watu kupumzika wakijivinjari kwa vinywaji na mlo, waandamanaji waliruhusiwa kuingia hadi jikoni kuzima makali yake.
Kilichotuliza moyo, ni kuona wahudumu wa Java wakiwalaki kwa ukarimu.
Langoni, mlinzi naye alikuwa akiwakaribisha kwa moyo mkunjufu.
Gen Z walionyesha ukomavu wa hadhi ya juu, wakiheshimu kanuni za mkahawa, na kinyume inavyoshuhudiwa katika maandamano mengi Kenya hawakutekeleza wizi wala uhalifu wowote.
Vijana hao watulivu, wachangamfu na wacheshi, walionekana kuwa kwenye simu zao katika kile kilionekana kama kufahamisha wenzao mitandaoni kuhusu yanayojiri.
Gen Z ni watumizi hodari wa majukwaa ya Tiktok, Instagram, X (awali Twitter), Facebook, Telegram na WhatsApp.
Safu hizo kila wanaposhiriki maandamano hujaa matukio ya siku, yakiwemo picha, video, na kauli zenye ucheshi.
Baada ya ukarimu wa Java, walikuwa wananunua bidhaa za kula na kunywa, na kurejea nyanjani kuelezea ghadhabu zao.
Huku wakishikilia kuwa hawana viongozi, hawaegemei mrengo wowote ule wa kisiasa wala ukabila, wanajihami kwa simu za kisasa za mkono, bendera na chupa yenye maji.
Hali kadhalika, wengi wao wana vibango vyenye maandiko ya ukombozi wa Kenya.
Mitaa iliyotawala maandamano, ilihinikiza nyimbo za kukomboa nchi na kumtaka Rais William Ruto awasikilize.
“Zakayo lazima ashuke,” akasema mmoja wa waandamanaji waliojisitiri Java House, Nairobi dhidi ya makali ya gesi ya vitoza machozi.
Aidha, Gen Z walikuwa wamesitisha maandamano kwa muda kuomboleza wenzao waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Dkt Ruto majuma kadha yaliyopita, alilazimika kusaliti amri ya kutekelezwa kwa Mswada wa Fedha 2024 kuwa sheria.
Alikataa kuutia saini licha ya Bunge la Kitaifa kuupitisha, akiagiza ufutiliwe mbali.
Mswada huo tata, ulikuwa na vipengele vinavyopendekeza nyongeza ya ushuru wa ziada (VAT).
Mazungumzo yaliyotarajiwa kufanyika Jumatatu, Julai 15, 2024 kati ya Rais na Gen Z, hata hivyo, hayakutekelezwa vijana wakihoji hawayataki hadi pale “Ruto atashuka”.
Rais, kwa upande wake anadai maandamano yanayoshuhudiwa yanafadhiliwa na baadhi ya mashirika, kwa lengo la kuyumbisha serikali yake.