Makala

Makala ya mwisho ya Macharia Gaitho kabla ya kukamatwa kwake

July 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

Hotuba ambayo Raila alifaa kutoa KICC alipokutana na Ruto, Na Macharia Gaitho

Ndugu yangu, Mheshimiwa Rais William Ruto. Kwamba nakutambua hivi kunaonyesha mabadiliko katika uhusiano wetu. Hapo awali sikutambua uhalali wako, nilikutaja katika matamshi yangu yote ya umma kama ‘Bw Ruto’ tu.

Unafika wakati ambao lazima tuweke makosa ya zamani nyuma yetu, na kusonga mbele. Tukio la leo linaashiria kutimia kwa mazungumzo tuliyoanzisha ili kusuluhisha tofauti zilizotokana na uchaguzi wa urais wa 2022 ambao ulikuwa na utata.

Tume ya uchaguzi iliyoundwa upya na kufanyiwa marekebisho ni muhimu kuelekea uchaguzi ambao siku zijazo utakuwa wa uwazi, uwajibikaji na unaoweza kuthibitishwa.

Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano inayojumuisha wawakilishi kutoka muungano wako unaoongoza, wa Kenya Kwanza, na muungano wetu wa upinzani, Azimio la Umoja-One Kenya, ilitoa mapendekezo mengine mengi, ambayo ni lazima kwa pamoja tuharakishe utekelezaji wake ili kusaidia kuharakisha kutimia kwa ndoto ambayo imekuwa vigumu ya jamii yenye umoja, amani na uhuru.

Lazima tukubali, hata hivyo, kwamba hali imebadilika sana tangu makubaliano ambayo yanatukusanya hapa leo yalipoafikiwa.

Mheshimiwa Rais, utakumbuka kwamba masuala ya awali yaliyoibuliwa na maandamano ya Azimio yalihusu gharama ya maisha. Tulipofanya mazungumzo ya kusitisha mapigano, hata hivyo, upande wako ulisisitiza kwamba ushuru mkubwa usiwekwe mezani kwani hilo lilikuwa suala la kushughulikiwa na serikali kulingana na sera na programu zake yenyewe. Tulikubali shingo upande, na kwa kweli tukakuacha ujipike kwa mafuta yako mwenyewe.

Mheshimiwa Rais, hali sasa ndio hii. Uasi wa Gen Z umechochewa na wasiwasi ulioenea miongoni mwa umma kuhusu gharama ya maisha, pamoja na masuala mengine mazito, ikiwa ni pamoja na chuki iliyoenea juu ya tabaka lako tawala kuonyesha utajiri uliopatikana kwa njia isiyo halali; kutapika kwa viatu vya raia wenye njaa, chembilecho aliyekuwa Balozi wa Uingereza jijini Nairobi.

Ni hali ya kututia wasiwasi sote, lakini ni kizazi cha vijana ambacho si mateka wa migawanyiko ya kawaida ya vyama vya siasa ambao wamechukua mkondo wao kwa nguvu za kustaajabisha.

Pale tuliposhindwa au kukata tamaa, watoto na wajukuu wetu wamechukua uongozi, na wamefanikiwa katika wiki chache kuliko jinsi mtu yeyote angeweza kufikiria.

Wameunganisha nchi nzima kupinga kutozwa ushuru. Wamevunja imani potofu kwamba kuchukua hatua za raia ni lazima ufadhiliwe na wanasiasa. Wameliamsha taifa. Wameaibisha viongozi wa kidini warudi kwenye wito wao. Wameshinda kiburi cha madaraka. Hofu imekwisha.

Vijana wetu wamefanya Kenya kutambuliwa kimataifa. Wameteka hisia za vijana kila mahali, ambao kwa hakika watakuwa wakiiga Wakenya.

Tumekusanyika hapa leo kusherehekea matunda ya mazungumzo. Tunashukuru uko tayari kusikiliza na kuweka mifumo ya mazungumzo ya kitaifa. Hata hivyo, ni lazima pia usikilize sauti zote.

Hayawezi kuwa mazungumzo yanayoendeshwa na kudhibitiwa na wanasiasa kupanga kugawana madaraka. Sisi katika Azimio tumejitolea kufanya mazungumzo lakini lazima tuseme tena ili kuepuka shaka kwamba hatuko tayari kujumuishwa katika serikali. Wajibu wetu mtakatifu kama upinzani mwaminifu ni jukumu la kuiwajibisha serikali. Kitu kingine chochote kitakuwa usaliti kwa watu.

Kwa hiyo, masuala ya serikali ya umoja wa kitaifa au kitu cha aina hiyo hakitajadiliwa.

Hatimaye Bw Rais, na Wakenya wenzangu, sisi ambao tumejitolea maisha yote kupigania haki ya kijamii, kiuchumi na kisiasa lazima tuchukue hatua zetu mapema. Tunaweza kuondoka tukiwa na imani kwa kujua kwamba mapambano hayajakuwa bure, kwa kuwa tuna warithi wanaostahili katika kizazi kipya cha wapiganaji.

Tunakumbushwa kwamba mapambano ya kutumia silaha kupigania uhuru yalianzishwa katikati ya miaka ya 1940 na vijana wa kiume na wa kike ambao bado walikuwa matineja, ambao walikaidi machifu na makanisa yaliyolazimishwa kwa watu na wakoloni.

Tunakumbuka kwamba watu weledi waliokuja kuwa mawaziri wa kwanza wa Baraza la Mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wakuu wa mashirika ya umma baada ya kupata uhuru 1963, wengi wao walikuwa katika miaka ya ishirini na thelathini. Na kwa kweli hatuwezi kusahau viongozi vijana maarufu Young Turks ambao waliongoza vita dhidi ya udikteta wa chama kimoja kutoka 1990.

Kutokana na historia hiyo fupi tunaona kwamba uasi wa Gen Z leo unafuata historia na mila za kuonewa fahari. Vijana wamekomboa nafasi zao. Sisi kama wazazi au viongozi tunaweza kutoa mwongozo, msaada na kutia moyo, lakini hatufai kuthubutu kuwazuia kwa sababu tutasukumwa kando na wimbi kubwa wanalovumisha.

Imetafsiriwa na Benson Matheka