Kimataifa

Biden asitisha kampeni baada ya kuugua Covid shinikizo zikizidi ajiondoe katika uchaguzi

Na MASHIRIKA July 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WASHINGTON DC, AMERIKA

RAIS wa Amerika Joe Biden anakabiliwa na shinikizo mpya kujiondoa katika uchaguzi wa urais huku kampeni zake zikisitishw baada ya kuambukizwa virusi vya Covid 19.

Msemaji wa Ikulu ya Amerika White House, Bi Karine Jean-Pierre alisema tayari Biden alipata chanjo ya ugonjwa huo pamoja na ile ya kuongeza nguvu, japo hali yake sio njema.

White House ilisema Bw Biden atarejea katika makazi yake ya kibinafsi huko Delaware ambapo atajitenga huku akiendelea kutekeleza majukumu yake .

“Rais ataendelea kutekeleza majukumu yake yote wakati huu, akiwa nyumbani kwake,” alisema Bi Jean-Pierre.

Hali hiyo ilimpata kiongozi huyo, alipokuwa akifanya kampeni huko Nevada, akitafuta uungwaji mkono ili kuchaguliwa tena Mwezi Novemba 2024.

Mapema Jumatano, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 81, aliwatembelea wafuasi wa chama chake huko Las Vegas na kuzungumza katika hafla iliyokuwa imeandaliwa.

Hata hivyo, alisitisha hotuba yake katika jimbo hilo ambalo lina nguvu sawa za ushawishi kati ya chama chake cha Democrats na kile cha Republican.

Kampeni ya uchaguzi wa Rais huyo inaonekana kwenda kinyume na ilivyotarajiwa. Maambukizi hayo yakichangia kukabiliwa na shinikizo la kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea urais kutokana na umri wake.

Vyombo vya habari nchini humo viliripoti kuwa Kiongozi wa walio Wengi katika Seneti, Bw Chuck Schumer na Kiongozi wa walio Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Hakeem Jefferies, ambao ni Wanademokrasia wawili wakuu katika Bunge la Amerika, kwa nyakati tofauti walikutana na Bw Biden faraghani.

Wawili hao, walielezea kuwa na wasiwasi mkubwa kwamba huenda mgombea wao wa chama cha Democrats akaathiri vibaya ushindani katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Daktari wa rais huyo, Bw Kevin O’Connor, alisema Bw Biden alikuwa na dalili za matatizo ya kupumua, ikiwa ni pamoja na mafua na kikohozi na alipewa dozi yake ya kwanza ya Paxlovid.

“Bw Biden alijihisi vizuri wakati wa hafla yake ya kwanza ya siku hiyo, lakini baadaye akapatikana kuwa na maambukizi,” alisema Dkt O’Connor.

Baadaye Bw Biden alitumia mtandao wa X ambao zamani ulijulikana kama Twitter, kumshukuru kila mtu ambaye alimtakia mema.

“Nitahakikisha kazi inafanyika kwa watu wa Amerika wakati ninaendelea kupona,” aliandika Bw Biden.