Habari za Kitaifa

SIKIO LA KUFA? Wabunge ODM wafunguka walionya Raila kwamba kujiunga na serikali ni sumu

Na RUSHDIE OUDIA July 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MKUTANO wa Kundi la Wabunge wa ODM (PG) ulishindwa kufikia uamuzi kuhusu pendekezo la kujiunga na serikali ya Rais William Ruto ya Kenya Kwanza.

Baadhi ya waliohudhuria waliambia Taifa Leo kwamba baada ya Katibu Mkuu Edwin Sifuna kusoma maazimio ya Kamati Kuu ya Usimamizi, kiongozi wa chama Raila Odinga pia alimtaka Gavana wa Siaya James Orengo kutoa mtazamo wake baada ya kuonya kuwa kujiunga na serikali ya Ruto ni sumu.

Waliohudhuria wanasemekana kuidhinisha masharti ya awali ya Gavana Orengo kabla ya kukubali kufanya kazi na Ruto, ambayo walikubali kuwa yanafanaba na yale ya Gen Z.

Katika mahojiano, Bw Orengo alieleza kuwa wasilisho lake lilikuwa na ‘masharti yasiyoweza kupunguzwa’ ambayo chama cha ODM na muungano wa Azimio la Umoja One Kenya wanasema lazima yatimizwe ili mazungumzo yoyote yafanyike.

Baadhi ya masharti hayo yaliidhinishwa na Kamati Kuu ya Usimamizi ya chama hicho ili kuweka mazingira mazuri ya Mkutano Mkuu wa Kitaifa.

Kulingana na Bw Orengo, vijana wa Kenya wanapaswa kuruhusiwa kuendeleza maandamano ya amani jinsi katiba ya Kenya inavyoruhusu.

Ukatili wa polisi, ikiwa ni pamoja na utumiaji wa risasi halisi na vitoa machozi dhidi ya waandamanaji, lazima pia uepukwe kwa mujibu wa amri ya mahakama iliyotolewa mwezi uliopita.

Masharti mengine yaliyowekwa na Bw Orengo ni pamoja na kuondolewa kwa mashtaka na kuachiliwa bila masharti kwa wale waliokamatwa wakati wa maandamano ya hivi majuzi na mwaka jana.

“Tunataka familia za waliouawa au kujeruhiwa wakati wa maandamano ya mwaka jana walipwe ipasavyo. Walio na bili za hospitali zinapaswa kufutwa na wale waliopoteza mali yao pia walipwe,” alisema Bw Orengo.

Pia alitaka hatua zichukuliwe dhidi ya makamanda wakuu wa polisi na aliyekuwa waziri Kithure Kindiki kwa kusimamia vifo na kujeruhiwa kwa waandamanaji wasio na hatia.

“Kabla ya mazungumzo ya aina yoyote, tunataka maafisa wa polisi waliofanya vitendo vya ukatili na mauaji wakamatwe na kufunguliwa mashtaka. Kufutwa kazi kwa Inspekta Jenerali Japheth Koome hakutoshi, tunataka mkuu wa polisi eneo la Nairobi Adamson Bungei atimuliwe na wote akiwemo Bw Kindiki kushtakiwa,” gavana wa Siaya alisema.

Bw Orengo aliambia Taifa Leo kwamba sharti lingine muhimu alilopendekeza ni kutaka kusitishwa mara moja kwa ushuru ulioanzishwa baada ya kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024, kama vile Ushuru wa Ukarabati wa Barabara na mwingine ambao huenda ukawaumiza Wakenya.

Alisisitiza kuwa lazima kuwe na muda wa kutimiza masharti na kwamba majadiliano au maazimio yoyote yanayofikiwa ni lazima yawekwe kwenye sheria na Katiba ili Mkutano Mkuu wa Taifa usiishie kuwa gumzo tu.

Muda mfupi baada ya wasilisho hilo, mnamo Jumatano, Wabunge na Maseneta wote walifunguka na kueleza wasiwasi wao, wakimtahadharisha Bw Odinga kwamba huu si wakati wa kutumia matukio ya sasa ili kumsikiliza Dkt Ruto ilhali hajakuwa na msimamo wa dhati, ikiwa ni pamoja na Mazungumzo ya Kitaifa.

Wabunge hao walimuonya Bw Odinga asiangukie mtengo wa Rais Ruto.