Maandamano yalazimu watalii kusitisha safari zao kuja Kenya
SEKTA ya utalii mjini Mombasa huenda ikazidi kudorora iwapo maandamano dhidi ya serikali yataendelea.
Wadau katika sekta hiyo wamesema utalii hutegemea amani na huenda idadi ya watalii ikapungua iwapo hali ya utulivu haitashuhudiwa.
Tayari baadhi ya hoteli zinasema asilimia 30 ya wageni wamefuta ziara zao wakihofia utovu wa usalama.
Meneja wa mauzo katika hoteli ya Travellers , Carolynne Kurumei alisema kuwa hali hiyo imewalazimu kuwashawishi watalii angalau kubadili tarehe za ujio wao ili kupunguza idadi ya wale wanaoahirisha safari zao za kutembelea Kenya.
“Tumeathiriwa sana na haya maandamano huku wageni wakihofia kuja Mombasa kwa mapumziko na hata mikutano,” alisema Bi Kurumei.
Idadi ya wageni wapya kutoka mataifa ya nje kutaka kuzuru humu nchini pia imeenda chini kwa kiasi kikubwa.
Mmoja wa washikadau katika sekta hiyo Mohammed Hersi, asema picha za kuogofya za utekaji nyara, mauaji na vurugu zinazopepereshwa hewani kutoka humu nchini zimewatia hofu wageni.
Maswali
“Watalii wanajiuliza kwa nini tuzuru Kenya wakati wenyeji hawana amani kwa sababu wanaona yote yanayojiri kwenye runinga zao,” alisema Bw Hersi.
Kaunti ya Mombasa ni kitovu cha utalii hasa msimu huu wa likizo na sherehe. Wenye hoteli hutazamia kuvuna pakubwa kuanzia mwezi huu wa Julai na Septemba.
“Tunaomba tu amani hali irejee kawaida kwani tunaelekea msimu wa sherehe na iwapo haya maandamano hayatasitishwa basi kutakuwa na kizungumkuti kupata wageni katika hoteli zetu, ” alisema Bi Kurumei.
Katika hoteli ya Sarova Whitesands, meneja mkuu Francis Msengeti , anakiri kwamba kumekuwepo na wageni waliobadili tarehe za ujio wao ila takwimu zinaonyesha kuwa wengi wangetaka kuja ila hali ya maandamano imewaweka njia panda.
“Tumeona wageni wakiahirisha safari zao baada ya kuagizia nafasi lakini tumeona pia wengi wao wangetaka kuja Mombasa kukamilisha likizo au mikutano yao,” alisema Bw Msengeti.