Habari za Kitaifa

Mhudumu wa usafi katika magereza ashtakiwa kupokea Sh300 milioni kwa ‘kuuza hewa’


MFAGIAJI katika idara ya Magereza Eric Kipkirui Mutai ameshtakiwa kwa ulaghai wa Sh301 milioni kwa kutoa huduma ‘hewa’.

Msemo ‘kuuza hewa’ hutumiwa kueleza hali kwamba mtu analipwa pesa kwa huduma au bidhaa ambazo hazikuwasilishwa.

Mutai, anayemiliki kampuni kadhaa zilizolipwa pesa hizo alishtakiwa katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi pamoja na wakuu katika Idara ya Magereza.

Mutai alishtakiwa pamoja na Mageto Omari Mirieri, afisa mkuu masuala ya fedha Sarah Kemunto Kerandi, mhasibu mkuu Joseph Kamau, Moses Juma Sirengo na mfanyabiashara Maureen Ndungwa Mwikya.

Ndungwa ni mkurugenzi wa kampuni ya Reenn East Africa Company iliyolipwa mamilioni ya pesa kwa kuuzia idara ya magereza ‘hewa’

Kamishna Mkuu wa Idara ya Magereza Benjamin Obuya Njoga pamoja na washukiwa wengine saba hawakufika kortini na waliamriwa wajisalimishe mara moja.

Wameagizwa wafike kortini Julai 22, 2024 kujibu mashtaka dhidi yao.

Njoga atashtakiwa pamoja na Joseph Kamau Mwangi, Humphrey Wende Abok, James Nyang’au Gekobe, Joseph Ochoki Omaiyo, Joseph Kariuki Mwangi (T/AJoslil General Supplies), Stephen Kisonzo Mulwa (T/A Castro Supplies and Stemu Supplies) na Mulwa Farm Limited.

Mutai na wenzake walikana mashtaka 68 ya kula njama za kuilaghai serikali, kutumia mamlaka ya afisi zao vibaya na kushiriki ulanguzi wa pesa za umma.

Mutai alikana mashtaka dhidi yake aliposhtakiwa pamoja na Mageto Omari Mirieri, Sarah Kemunto Kerandi, Joseph Kamau, mhasibu Moses Juma Sirengo na Ndungwa.

Hakimu aliwaachilia kwa dhamana ya Sh4 milioni pesa tasilimu kila mmoja baada ya kiongozi wa mashtaka Celestine Oluoch kusema DPP hapingi washtakiwa wakiachiliwa kwa dhamana.

Kila mmoja aliachiliwa kwa dhamana ya Sh4 milioni pesa tasilimu hadi Agosti 1, 2024.