Habari za Kitaifa

Sitawabembeleza tena, Rais Ruto sasa aambia Gen Z

Na FATUMA BARIKI July 21st, 2024 1 min read

RAIS William Ruto amesema amesikiza vya kutosha malalamishi ya vijana wa Gen Z na Wakenya wanaoandamana na kwamba imefikia wakati wa kusitisha mgogoro.

Akizungumza baada ya kuhudhuria ibada katika kanisa la AGC Chabango, Kaunti ya Bomet, Jumapili, Dkt Ruto alisema hataruhusu ghasia ziendelee kushuhudiwa nchini akisisitiza kwamba taifa hili ni la kidemokrasia.

“Waliniambia hawataki Mswada wa Fedha 2024, nikauondoa. Wakasema wanataka niongee nao kwenye jukwaa lao la X. Nilipoingia huko wakatoroka. Nikawaita kwa majadiliano ya kitaifa, pia hiyo wamekataa. Sasa imetosha, enough is enough,” akasema Rais Ruto.

Aliendelea kusema kwamba kama taifa, haifai kuondoa demokrasia na kuleta “udikteta wa watu ambao nyuso zao hazionekani, hawana kiongozi, hawana utambulisho.”

“Wanataka kutumia ghasia kuleta maafa na uharibifu wa mali.”

Akaendelea: “Kama serikali, tutakuwa imara kabisa kulinda maisha na mali ya watu. Hatutaruhusu ghasia kuendelea,” akasema Dkt Ruto kwa kile kinachofasiriwa kuwa serikali itafutilia mbali maandamano kwa njia yoyote ile.

“Naambia hao watu ambao wanachochea maandamano wakiwa mitandaoni, ambao wanafadhili ghasia na ukosefu wa amani wajitokeze na watuambie jinsi ya kuendeleza taifa letu mbele. Wasibakie tu bila kujitambulisha.”

Bw Ruto pia aligeukia vyombo vya habari na kuvitaka kutekeleza shughuli zao kwa uwajibikaji.

“Naomba wanahabari kuripoti kwa uwajibikaji, sio kuripoti kama kwamba wanasherehekea uharibifu wa taifa letu na maisha ya watu. Ikiwa nchi itaungua, hakuna kitu kitabakia kwenu kuripoti,” akasema.