Habari za Kaunti

Gavana motoni kuhusu Sh96 milioni

Na VITALIS KIMUTAI July 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Kaunti ya Bomet, Hillary Barchok, amejipata mashakani huku madiwani wakimwandama kuhusu Sh96 milioni za kufadhili maendeleo alizodai zimekuwa zimesambaziwa wadi 25 eneo hilo kila mwaka.

Madiwani hao sasa wametishia kutimua nusu ya mawaziri wa serikali ya kaunti hiyo baada ya Profesa Barchok kudai fedha hizo zilitumwa kupitia idara 10 katika wadi zilizopo maeneobunge ya Bomet Mashariki, Bomet ya Kati, Chepalungu na Sotik.

Diwani wa Wadi ya Ndarawetta, Dancel Kipngeno Kirui, na mwenzake aliyeteuliwa, Victor Rop, walimweleza Gavana waziwazi wikendi kwamba watawatimua mawaziri ili kuadhibu serikali ya kaunti hiyo kwa kuwagonganisha na wananchi.

Spika wa Bunge la Kaunti, Cosmas Korir, vilevile amewaongoza madiwani wanaoongoza kamati mbalimbali kutaja madai ya Gavana kama “yakupotosha na yanayopaswa kukosolewa.”

“Wewe (Barchok) umetuweka mtegoni kwa kudai wadi zetu zilipokea Sh96 milioni za maendeleo. Watu wanatuuliza maswali tusiyoweza kujibu kwa sababu miradi hiyo haipo. Jibu maswali hayo sasa kwa sababu uko hapa na wapiga kura wapo miongoni mwetu,” alisema Bw Kirui.

“Nataka kukuhakikishia kama bunge, tumeafikiana kukabiliana na mawaziri katika serikali yako. Tutawaita na kuanzisha mchakato wa kuwatimua. Wewe ni rafiki yangu, lakini sio kwa hili, nakwambia tutafanya hivyo,” aliongeza Bw Kipngeno.