Hofu fisi wakizurura ovyoovyo Kitengela
WAKAZI wa Kitengela Kaunti ya Kajiado wamekuwa wakiishi kwa hofu kwa muda wa wiki mbili zilizopita kutokana na fisi wengi kuzurura ovyoovyo mtaani humo hasa nyakati za usiku.
Fisi hao wanashukiwa wametoka kwenye mbuga ya wanyama ya Nairobi na walionekana wakizurura mitaa ya Namelock, Upper Milimani, Acacia nyakati za usiku.
Baadhi ya wakazi pia wameona wanyama hao wakila mizoga nyakati za usiku na kusababisha taharuki zaidi. Punda wawili, mbuzi kadhaa wameripotiwa kuuawa na wanyamapori katika eneo hilo japo hakuna kisa cha binadamu kuvamiwa ambacho kimeripotiwa.
Mkazi Moses Njuguna ameambia Taifa Dijitali kuwa alikumbana na fisi alipokuwa akiendesha gari kuelekea nyumbani kwake mtaa wa Upper Milimani usiku.
“Nilikumbana na fisi hao barabarabani nikienda nyumbani na licha ya kuongeza mwangaza zaidi wa taa ya gari, hawakutishika. Niliendesha gari polepole nyuma yao hadi wakatokomea na nilikuwa nimeogopa sana,” akasema Bw Njuguna.
Wakazi sasa wamesema hawatembei sana usiku kwa hofu ya kuvamiwa na fisi hao.
“Hatuko salama hapa na ni hatari zaidi kutembea usiku kwa hofu ya kuvamiwa na fisi au wanyama wengine wa porini,” akasema mkazi George Riri.
Wenyeji hao sasa wametaka Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Nchini (KWS) kuwahamisha wanyama hao hadi mbuga ya wanyama ya Nairobi ama mbuga nyingine.
Mtaa wa Kitengela umekuwa ukishuhudia visa vingi vya mzozo kati ya wanyamapori na binadamu kutokana na ukaribu wake na mbuga ya wanyamapori ya Nairobi. Ndovu, simba na swara ni kati ya wanyamapori ambao wamekuwa wakisumbua wakazi mtaani humo.