LSK: Serikali iliongeza ushuru wa ukarabati wa barabara kinyume cha sheria
CHAMA cha Mawakili Nchini (LSK) kimekashifu serikali kwa kuongeza kodi ya ukarabati wa barabara (RML) licha ya kuahidi ushuru hautaongezwa, baada ya shughuli ya ukusanyaji maoni ya umma.
Katika taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Kawi na Petroli (EPRA) mnamo Julai 14, 2024, bei ya mafuta ilishuka kwa kiwango kidogo sana lakini RML ikaongezeka kutoka Sh18 hadi Sh25.
“Hatua hii inakinzana na hakikisho ya aliyekuwa Waziri wa Barabara na Uchukuzi, Kipchumba Murkomen ambaye, katika taarifa rasmi ya Julai 8, 2024, aliwahakikishia Wakenya kuwa ushuru hautaongezwa,” alisema Rais wa LSK, Faith Odhiambo kupitia taarifa Jumatatu.
Tangazo la Bw Murkomen lilisema: “Kama ilivyopendekezwa na Wakenya, tutaongeza RML wakati tuna uhakika na kuwa mikakati yoyote ya mapato haiwezi kusababisha ongezeko la gharama ya maisha.”
Kabla ya ushuru huu kupanda, zoezi la kukusanya maoni ya umma lilifanywa katika sehemu tofauti nchini Wakenya wakipinga mpango huu.
LSK inalalama kuwa serikali imepuuza maoni ya Wakenya na kanuni za Katiba kwa kutupilia mbali maoni yao bila maelezo.
“LSK inaona hatua hii kuwa ya nia mbaya na isIyoheshimu Katiba. Inakosa kuzingatia kanuni za uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa umma kama zilivyoainishwa katika Katiba yetu,” alisema Bi Odhiambo.
Rais wa LSK aliendelea kuteta akikemea serikali kwa kutokuwa wazi na kutotangaza nyongeza hii ya ushuru kupitia gazeti rasmi la serikali.
Hata hivyo, Bi Odhiambo ameeleza kuwa hata kama serikali itachapisha mabadiliko haya, haitakuwa imefuata sheria inavyofaa.
“LSK inataka serikali iondoe nyongeza ya kodi iliyowekwa kinyume cha sheria, la sivyo tutachukua hatua zifaazo kushinikiza serikali kuheshimu Katiba kikamilifu,” alifoka Rais huyo wa LSK.