Habari za Kitaifa

Setilaiti kutambua changamoto za mimea shambani

Na CHARLES WASONGA July 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAPEMA mwaka huu, 2024, Kenya iliandikisha historia kwa kuzindua Setilaiti yake ya kwanza angani na kuwa taifa la pili Barani Afrika kufanya hivyo baada ya Misri.

Setilaiti hiyo kwa jina, Taifa-1, na iliyotengenezwa na wahandisi wa Kenya, ilizinduliwa katika kituo cha usafiri wa wa anga wa Vandenberg jijini Carlifonia, Amerika kwa kutumia roketi aina ya Falcon-9 ya kampuni ya SpaceX.

Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi na Shirika la Anga la Kenya (Kenya Airspace Agency), chombo hicho kitapiga jeki utafiti wa angani na kusaidia katika ukusanyaji wa data ambazo zitakatumika katika tafiti zitakazoisaidia serikali kuratibu mipango ya maendeleo

Aidha, setilaiti hii imekuwa ikitumika kwenye sekta ya kilimo kwa sababu ajili ya kukusanya data na picha, muhimu kufanikisha utafiti wa kilimo.

Pattern Odhiambo, ambaye ni mtaalamu katika masuala ya Setilaiti anasema kuwa Taifa-1 vilevile inasaidia kuchunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa sekta mbalimbali za kilimo nchini.

“Setilaiti hii inaweza kutambua mabadiliko katika mazao shambani na mimea mingine kwa kipindi kirefu. Kwa njia hii wataalamu wanaweza kubashiri viwango vya mavuno sehemu kote nchini,” anasema

Kulingana na Odhiambo, data zinazokusanywa na chombo hiki, na kuhifadhiwa kwa mfumo wa kidijitali, zitaisaidia serikali kuratibu mikakati ya kuimarisha uzalishaji wa chakula.

“Data zitakazokusanywa na Taifa-1 zitazisaidia asasi za kuendesha tafiti kuhusu kilimo kama vile Shirika la Utafiti kuhusu Kilimo na Ufugaji (KARLO), ili ziweze kutoa ushauri sahihi kwa wakulima kuhusu mbinu za bora za kilimo na aina za mimea inayoweza kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali nchini,” anaeleza.

Odhiambo anaongeza kuwa teknolojia ya setilaiti itawezesha wakulima kubaini shida halisi zinazoathiri mashamba yao, kama vile maambukizi ya magonjwa na wadudu waharibifu, na sehemu ya shamba zilizoathirika ili wachukue hatua haraka.