Habari za Kitaifa

Vijana wakaidi onyo la Ruto na kuandamana, ila wakutana na makundi yanayotetea Serikali

Na WAANDISHI WETU July 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAANDAMANAJI wanaopinga serikali ya Kenya Kwanza, Jumanne walikaidi onyo la Rais William Ruto na kujitokeza barabarani katika miji mbalimbali kumtaka ajiuzulu.

Jumapili Kiongozi wa Nchi alionya kuwa serikali imevumilia vya kutosha waandamanaji na akaapa kuwakabili vikali.

Kufikia saa sita mchana jana, maandamano yalikuwa yameripotiwa katika kaunti za Embu, Mombasa, Kisumu, Nairobi, Homa Bay, Nyeri, Lamu, Kisii na Kajiado.

Lakini tofauti na maandamano ya awali, jana makundi yanayounga mkono serikali yaliibuka kukabiliana na wanaompinga Rais Ruto jijini Nairobi na Karatina, Nyeri – wakiendesha pikipiki kuunga mkono utawala wa Kenya Kwanza.

Kikundi kilichojumuisha waendeshaji boda boda, kiliingia katikati ya jiji la Nairobi kikipiga honi na kuimba nyimbo za kumuunga mkono Rais.

Watu hao wanaounga serikali waliruhusiwa na polisi kupita vizuizi vyote barabarani, wakibeba mabango ya kuunga mkono serikali yakiwa na maandishi kama Tumpe rais wetu wakati, Ruto tuko nyuma yako na Tumechoka na Gen-Z.

Wahudumu hao wa bodaboda ambao walifuatana na madiwani kadhaa wa Bunge la Kaunti ya Nairobi wanaounga mkono chama cha Dkt Ruto (UDA) – akiwemo Mark Mugambi (Umoja Mmoja) na Brian Itenya (aliyeteuliwa) – walionekana kupangwa vyema na kufadhiliwa.

Kwanza, walijaza mafuta pikipiki zao katika vituo vilivyoteuliwa vya petroli Jijini kabla ya kukusanyika katika bustani ya Uhuru Park, mojawapo ya maeneo yenye ulinzi mkali katika jiji, kupata mwelekeo.

“Kikundi kikubwa cha bodaboda kimefika katika Rubis, Haile Selassie. Wameambiwa wajipange kujaza mafuta, kuna mtu analipa. Polisi wa kutuliza ghasia walisimama karibu na kuwapuuza,” mwanahabari Robert Nagila aliandika katika X.

Wakati mmoja, kundi linalomuunga mkono Ruto lilikabiliana na waendeshaji bodaboda wengine karibu na Hoteli ya Hilton baada ya waendeshaji hao kuwatuhumu kwa uporaji.

Video zilizonaswa na watazamaji zilionyesha watu waliokuwa kwenye magari ya kifahari wakiwapa pesa taslimu waendeshaji bodaboda waliokuwa wakiunga mkono upande wa serikali.

Takriban pikipiki tatu ziliteketezwa kwenye barabara ya Kenyatta Avenue na Haille Selassie huku makundi mawili yakipigania haki ya kuandamana.

“Polisi walifyatua vitoa machozi kuzima mapigano hayo. Kundi kama hilo, lililopewa jina la Amani Kenya, lilikabiliana na waandamanaji dhidi ya serikali Imara Daima kwa kuwasaidia polisi.

Katika mji wa Kitengela, Kaunti ya Kajiado, watu 10 walikamatwa wakiandamana. Polisi waliwarushia waandamanaji vitoa machozi huku wakisaidiwa na helikopta kupiga doria.

Jijini Kisumu, watu wawili walijeruhiwa walipofyatuliwa risasi na polisi wakikabili waandamanaji waliofunga barabara kuu ya Nairobi Kisumu mjini Ahero.

Mwanaharakati Boniface Ogutu Akach, alikamatwa na polisi alipojiunga na waandamanaji jijini Kisumu.

Homa Bay, polisi walitumia mabomu ya machozi na risasi kuwatawanya waandamanaji.

Mjini Mombasa, kulikuwa na makabiliano kati ya waandamanaji na polisi katika barabara ya Moi Avenue baada ya polisi kuwaamuru kutawanyika, wakidai hawakuwa wamearifu maafisa wa usalama kabla ya maandamano hayo.

Maafisa hao walirusha mabomu ya machozi kuvunja maandamano, na kumjeruhi mfanyabiashara ambaye alikimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Mkuu wa Polisi, Kaunti ya Mombasa Maxwell Agoro alijaribu kusimamisha maandamano hayo akieleza kuwa walikuwa wakivunja sheria.

Hata hivyo, waandamanaji hao walisisitiza kuendelea na maandamano hayo, wakihakikisha kwamba hawatamdhuru mtu yeyote. Dakika chache baadaye, maafisa wa polisi walirusha vitoa machozi kuwatawanya.

Maafisa waliovaa barakoa wakiwa katika magari yenye nambari zilizofunikwa, mara kwa mara walirushia vitoa machozi kila gari lilipopita eneo la Casablanca.

Ripoti za Harry Misiko, Kevin Cheruiyot, Ngina Kirori, Mercy Simiyu, Millicent Mwololo, Stanley Ngotho, Sammy Kimatu, Rushdie Oudia, Brian Muchiri, Jurgen Nambeka, Wycliffe Nyaberi, George Odiwuor na Melvin Odhiambo