Maoni

Baada ya sarakasi za siasa za Kenya, uhondo sasa upo Amerika

Na DOUGLAS MUTUA July 27th, 2024 2 min read

NIRUHUSU nitanue kifua kidogo: Kwa Jumamosi mbili zilizopita, nimetabiri mambo kwenye ukurasa huu na hatimaye yakatokea.

Usiniulize nilijuaje yangetokea, hata mwenyewe sijui, ila yamkini nina nyota ya masuala ya kisiasa yanayofanyika Kenya na duniani kwa jumla.

Sijazoea kuringa, hivyo maringo nitayafikisha hapo, lakini sharti nikukumbushe kwamba nilipopendekeza Rais William Ruto alifute baraza zima la mawaziri, niliamka siku iliyofuata nikapata amewapiga kalamu wote.

Vilevile, wiki jana nimekutabiria kuwa Rais wa Amerika, Joe Biden, huenda akajiengua kutoka kinyang’anyiro cha kutetea wadhifa wake kitakachofanyika Novemba, na amekwisha kufanya hivyo.

Uamuzi huo pekee umebadili mkondo wa siasa za Amerika ghafla! Propaganda dhidi ya uzee wake si hoja tena kwa sababu hawanii urais; inatarajiwa kumwathiri aliyekuwa mpinzani wake mkuu, na mzee mwenzake, Bw Donald Trump, 79.

Nakuandikia haya nikiwa na furaha isiyokuwa na kifani kwa sababu ya msisimko wa kisiasa ninaoushuhudia huku Amerika, nchi ya walio huru kwa sababu ya walio jasiri.

Mambo yamebadilika ghafla kikweli, siasa zimeanza kupendeza tena, upo ushindani wa kweli, sikwambii cheche kali za matusi ya kisiasa zinafyatuka kotekote!

Kujiondoa kwa Rais Biden kumeathiri hali pakubwa kwa kuwa amependekeza makamu wake, Bi Kamala Harris, ateuliwe na chama cha Democrat ili kumkabili Bw Trump, mbeba mwenge wa kile cha Republican.

Bw Trump na kundi lake, ambao walitia dua kimya-kimya Mzee Biden asalie kwenye kinyang’anyiro ili wamponde na kumfanya unga kwa raha zao, wapo katika hali ya kukanganyikiwa.

Hawakutarajia kwamba mwanamke aliye mseto wa mtu Mweusi na Mhindi anaweza kuwa mwaniaji wa chama kikuu kama Democrat na kuungwa mkono kwa mapana na marefu.

Saa chache tu baada ya Rais Biden kumpendekeza Bi Harris, rais wa zamani wa Amerika, Bill Cinton, na mkewe, Hillary, walitangaza wazi kwamba wanamuunga mkono Bi Harris. Watu wengine mashuhuri walifuatia kutoa tangazo hilo na wanaendelea kufanya hivyo.

Hata wanasiasa wengine waliokuwa na nia ya kuwania urais kwa dhamana ya chama cha Democrat baada ya Bw Biden kujiondoa wameng’oa makucha na kumwachia Bi Harris kazi ya kumenyana na Bw Trump.

Na hatimaye aliyenguruma dakika za mwisho na kutetemesha chaka zima la siasa ni Mkenya-Mmarekani, Rais Mstaafu Barack Obama, ambaye ni mlezi wa kisiasa wa Bi Harris, alipotangaza Ijumaa kwamba hata yeye na mkewe Michelle, nao pia wanaunga mkono azma yake wakiapa kufanya kila wawezalo kuhakikisha anarithi Ikulu ya White House.

Inaaminika ni Bw Obama alimshawishi Bw Biden kujiengua kama mzalendo na shujaa wa kitaifa.

[email protected]