Umaarufu wa Harris wapaa na kumkaribia Trump huku Obama sasa akimwidhinisha
UMAARUFU wa mgombea urais wa chama cha Democratic Kamala Harris unatarajiwa kupanda hata zaidi baada ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa Rais wa zamani Barack Obama na mkewe, Michelle.
Kwenye video iliyoonekana kunaswa wakati wa shughuli za kampeni, Makamu wa Rais anajibu simu kutoka kwa Obama kupitia simu yake ya mkononi.
“Nakupigia kukuarifu kwamba ni fahari yangu na Michelle kukuunga mkono na tutafanya kila tuwezalo kukuwezesha kushinda uchaguzi huu na kuingia Ikulu,” Rais huyo wa zamani anasikika akisema.
Makamu wa rais huyo wa Amerika Alhamisi alisaka uungwaji mkono katika shirikisho kubwa zaidi la walimu nchini humo huku matokeo ya kura ya maoni yakionyesha anamkaribia rais wa zamani Donald Trump.
Kuibuka kwa Harris kama mgombea urais wa chama tawala cha Democrat baada ya kujiondoa kwa Rais Joe Biden, 81, kumeleta msisimko mpya katika kinyang’anyiro cha urais nchini Amerika.
Makamu huyo wa Rais anatarajiwa kuidhinishwa rasmi kuwa mgombea urais wa chama cha Democratic katika Kongamano la Kitaifa la chama hicho jijini Chicago, jimbo la Illinois mwezi ujao.
Harris atapambana na Trump wa chama kikuu cha upinzani Republican katika uchaguzi wa urais mnamo Novemba 5, mwaka huu.
Akihutubu jijini Houston katika Kongamano la Shirikisho la Walimu Amerika (FAT), Harris, 59, aliangazia zaidi sera za kiuchumi na haki za wafanyakazi.
Aliahidi kuendeleza mipango ya utoaji huduma nafuu za afya na utunzaji watoto.
Aidha, Harris aliwakashifu vikali viongozi wa chama cha Republican kwa kupinga utekelezaji wa sera ya kudhibiti umiliki wa bunduki kama njia ya kukomesha visa vya mashambulio ya risasi shuleni.
“Tunaongozwa na haja ya kupigania maisha mazuri siku zijazo,” Harris akauambia umati wa karibu watu 3,500.
“Tuko katika mapambano ya kupigania na kulinda haki za kimsingi na uhuru; haki za walimu wetu na watoto wetu,” akaongeza.
Baadaye zaidi ya wanawake 100,000 wa asili ya Waamerika weupe waliungana katika mtandao wa Zoom kuchanga pesa za kufadhili kampeni za Harris kando na kujadili mikakati ya kuendesha kampeni hizo.
Mchango huo unafuatia mwingine ulioendeshwa siku chache zilizopita na wanawake Weusi, wanaume Weusi na watu wa asili ya Latino.
Kura kadhaa za maoni zilizoendeshwa tangu Biden alipojiondoa katika kinyang’anyiro cha urais Jumapili iliyopita, ikiwemo kura ya Reuter/Ipsos, zinaonyesha kuwa Harris na Trump wanaanza kukaribiana kwa umaarufu.
Hii inaashiria kuwa wawili hao wataendesha kampeni kali zaidi katika muda wa miezi mitano na nusu ijayo.
Matokeo ya kura ya maoni yaliyoendeshwa na gazeti la New York Times na chuo cha Siena College na kuchapishwa Alhamisi yalionyesha Harris akimkaribia Trump, japo mgombeaji huyo wa Republican bado akiongoza.
Trump alikuwa mbele ya Harris kwa kuandikisha umaarufu wa asilimia 48 dhidi ya asilimia 46, miongoni mwa wapigakura waliosajiliwa.
Mapema mwezi huu wa Julai Trump alikuwa na umaarufu wa asilimia 49 mbele ya Biden aliyekuwa na umaarufu wa asilimia 41.
Hii ni baada ya Biden kufanya vibaya zaidi katika mdahalo kwa kwanza wa urais kati yake na Trump.
Ni kufuatia mdahalo huo ulioendeshwa na shirika la habari la CNN ambapo wafuasi wa chama cha Democrat walianza kumwekea Biden presha ajiondoe kinyang’anyironi.
Aidha, Harris alipata habari katika kura ya maoni katika majimbo matano muhimu nchini Amerika.
Kulingana na matokeo ya kura ya maoni yaliyochapishwa na Emerson College/The Hill, Makamu huyo wa Rais alianza kumkaribia Trump, kwa umaarufu katika majimbo kama vile: Arizona, Georgia, Michigan, Pennsylvania na Wisconsin.