Habari za Kitaifa

Mshangao mwanaume akimdunga kisu Kamanda wa Polisi kanisani

Na WYCLIFFE NYABERI July 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KAMANDA wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Kisii ya Kati Isaac Kimwele na waumini wengine wawili wa kanisa la Deliverance Church International Kisii walidungwa visu Jumapili asubuhi na mwanaume aliyejitosa kanisani humo wakati wa ibada.

Mwanaume huyo wa makamo anasemekana kuingia madhabahuni na kuanza kumkimbilia Mchungaji Peter Rotich, ambaye alikuwa akiendesha mahubiri ya ibada ya pili kwa lengo la kumchoma kisu.

Lakini wale waliokuwa karibu na mtumishi huyo wa Mungu walinyanyuka upesi kumzuilia.

Katika taharuki hiyo iliyositisha maombi kwa muda, Bw Kimwele na washirika hao wengine walidungwa visu. Kamanda Kimwele ni mshirika wa kanisa hilo.

Kanisa la Deliverance Church International Kisii ambako mwanamume alivamia na kujeruhi waumini, akiwemo kamanda wa polisi. Picha|Wycliffe Nyaberi

Kulingana na Bw Simon Onditi, ambaye ni mmoja wa walinzi wa kanisa, mwanamume huyo aliingia kanisani ibada ya pili ilipokuwa katikati.

“Alianza kujifanya kana kwamba ana uwazimu. Alikwenda kwenye madhabahu. Kwa kuwa madhabahu ni mahali patakatifu, nilisogea mbele kwenda kumtoa nje. Nilipojaribu kumshika, alianza vurugu na kunidunga kisu mkono wangu wa kushoto.

Alikuwa ameficha kisu hicho kwenye handikachifu aliyekuwa nayo katika mkono wake wa kulia kisha akaanza kukimbia,” Bw Onditi akasema.

“Jambo hili lilizua tafrani kubwa kanisani. Waumini wengine walipoona kilichotokea walikuja kunisaidia. Aliwachoma visu wale waliomkaribia kabla hajazidiwa nguvu,” akaongeza.

Simon Onditi, mmoja wa waliojeruhiwa kanisani Deliverance Church International Kisii akipokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH). Picha|Wycliffe Nyaberi

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kisii Charles Kases, alitembelea kanisa hilo na wale waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH). Alisema wao kwa kawaida huwapeleka baadhi ya maafisa katika kanisa hilo ili kudumisha amani endapo kutatokea tukio lolote kutokana na ombi lililoletwa na wasimamizi wake.

Watatu hao walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini katika hali nzuri.

Afisa huyo wa polisi alisema maafisa waliokuwa wametumwa katika kanisa hilo walifanikiwa kumkamata mtu huyo alipokuwa akijaribu kutoroka. Bw Kases aliongeza kuwa mwanamume huyo alikuwa amevalia barakoa na miwani.

Mtu mwingine aliyejeruhiwa alitambuliwa kwa jina la Francis Makori.