Habari za Kitaifa

Serikali yakataa kusajili chama cha Gen Z

Na COLLINS OMULO July 29th, 2024 2 min read

JARIBIO la watu fulani kusajili vyama vya kisiasa vyenye jina, Gen Z ili kuvuna kisiasa kutokana kampeni zilizoanzishwa na vijana kupigania uongozi bora nchini zimezimwa na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Nchini.

Msajili huyo, Anne Nderitu, wiki jana alifichua kwamba tangu msururu wa maandamano ya vijana hao wa kizazi cha sasa kuanza kwa kupinga Mswada wa Fedha wa 2024, afisi yake imepokea angalau maombi 20 kutoka kwa watu wanaotaka kuhifadhi majina ya vyama vya kisiasa.

Hata hivyo, alisema maombi hayo yote, yanayoanza na maneno Gen Z, yamekataliwa kwani yanakiuka sheria, haswa kipengele 91 (1) (a) (e ) cha Katiba kinachohusu masharti yanapasa kuzingatiwa kuunda vyama vya kisiasa.

“Hitaji la sheria ni kwamba kila chama cha kisiasa sharti kiwe na sura ya kitaifa na kiheshimu haki za watu kushiriki katika michakato ya kisiasa, yakiwemo makundi ya walio wachache na waliotengwa,” Bi Nderitu akasema.

“Kwa hivyo, licha ya kupokea zaidi ya maombi 20 kutoka kwa watu mbalimbali wakitaka tuhifadhi majina ya vyama vya kisiasa vinavyoanza na Gen Z, tumekataa maombi hayo kwa sababu yanakiuka Katiba,” akaongeza.

Bi Nderitu alisema afisi yake ilianza kupokea maombi hayo baada ya siku ya kwanza ya maandamano hayo, Juni 18, 2024 kutoka kwa watu waliotaka kutumia umaarufu wa wimbi hilo la maasi ya vijana kuvuna kisiasa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Watu hao walivutiwa na wimbi la vijana hao na hali kwamba hawakujinasibisha na kabila, kiongozi yeyote au chama chochote cha kisiasa.

“Chama cha kisiasa sharti kiwe na sura ya kitaifa na kijumuishe watu wa umri na matabaka yote. Sharti tuone watu wa umri wote katika chama cha kisiasa. Ukisema chama cha Gen Z, unaonekana kuwatenga watu wengine,” Bi Nderitu akaeleza.

Chama kinachoonekana kuwatenga watu wa umri fulani, msajili huyo anasema, basi chama hicho kinakosa sura ya kitaifa.

“Namna ambavyo, vijana hawataki kuachwa nje katika shughuli za vyama vilivyoko sasa au masuala ya uongozi, wao pia hawapaswi kuwaacha nje watu wengine. Kila mtu anafaa kushirikishwa, tangu hatua za kwanza kwa kubuni kwa chama chochote cha kisiasa,” Bi Nderitu akafafanua.

Kwa mfano ombi kutoka kwa Simon Maina Mwangi lilikataliwa na msajili wa vyama vya kisiasa kwa misingi hiyo hiyo ya kukiuka hitaji la kipengele cha 91 cha Katiba.

Bw Mwangi alitaka afisi ya Bi Nderitu kuhifadhi majina 10 ya vyama vya kisiasa ikiwa ni pamoja na; Gen-Z Movement, Gen Z National Movement, Gen Z People’s Alliance, Gen Z Peoples Movement, Gen Democratic Party, Gen Z Alliance Movement, Gen Z Democratic Movement, Gen Z United Movement, Gen Z Political Party na Gen Z Alliance Party.

Hata hivyo, Afisa huyo alikataa ombi hilo kupitia barua aliyomwandikia Bw Mwangi mnamo Julai 11, 2024.

Ombi jingine lililowasilishwa na John Onyango Ogenga, mnamo Juni 24 akitaka jina Gen Z lihifadhiwe pia lilikataliwa na Bi Nderitu kwa msingi huo huo.

Bw Ogenga sasa amewasilisha rufaa dhidi ya uamuzi huo katika Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa.

Anadai kuwa kukataliwa kwa ombi lake kunaenda kinyume na Katiba, kunaendeleza ubaguzi na kuhujumu haki zake za kisiasa.

Bw Mwangi pia ameapa kupinga uamuzi wa kukataliwa kwa ombi lake akidai sababu zilizotolewa na Nderitu hazina mashiko huku akitoa mfano wa chama cha Farmers Party kilichosajiliwa ilhali sio kila Mkenya ni mkulima.

“Kile nilitaka ni vijana wa Gen Z wawe na jukwaa ambako tunaweza kuangazia masuala yetu na kujitambulisha nayo. Watu wamekuwa wakituita magaidi au watu wasio na mwelekeo wala uongozi. Kwa hivyo, tunahitaji asasi ambayo imesajiliwa rasmi ili wenzetu waweze kujitambulisha nayo,” akasema Bw Mwangi, 32, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kiufundi Kenya (TUK).