BAHATI YA MTENDE: Kawira anusurika tena korti ikiamuru Njuri Ncheke itatue mzozo
BUNGE la Kaunti ya Meru jana lilipata pigo baada ya Mahakama Kuu kuahirisha uamuzi kuhusu hoja ya kumtimua Gavana Kawira Mwangaza na kuamrisha suala hilo lishughulikiwe na Baraza la wazee wa Njuri Ncheke.
Hii ina maana kuwa kuna uwezekano mkubwa Bi Mwangaza atanusurika nia ya kutimuliwa na madiwani kwa mara ya nne kwa sababu kisheria madiwani walikuwa na makataa ya hadi leo kuijadili hoja hiyo.
Kisheria, hoja ya kumbandua gavana inastahili kujadiliwa siku 10 baada ya kuwasilishwa kwake bunge la kaunti.
Bi Mwangaza alikuwa amesema kuwa hoja hiyo ilikuwa hafifu kwa sababu baadhi ya saini zilighushiwa, hakusikizwa na baadhi ya masuala yaliyojumuishwa yalikuwa kortini.
Jaji Linus Kassan Jumatatu alitoa amri ya kuzima hoja hiyo na kusema atatoa uamuzi wake mnamo Agosti 20.
“Njuri Ncheke ambalo ni baraza la juu la wazee Wameru linaamrishwa liwasilishe ripoti yake ya kupatanisha pande zote mbili jinsi ilivyoamrishwa na Rais wa Kenya. Wanastahili kuwasilisha ripoti hiyo kwa muda usiozidi wiki tatu kutoka sasa,” akasema Jaji Kassan.
Pia aliamrisha pande zinazozozana kufika mbele ya Njuri Ncheke kabla ya Jumatano wiki hii ili kusuluhisha utata kati ya madiwani na uongozi wa kaunti.
Amri hiyo ya korti ilitolewa kwa msingi kuwa Bi Mwangaza alisema hoja ya kumtimua ilikuwa inavuruga juhudi za upatanishi ambazo zimekuwa zikiendelea.
Mnamo Aprili, uhasama wa kisiasa kati ya gavana na bunge la kaunti ulipofikia kilele, wazee wa Njuri Ncheke na viongozi wa kidini kutoka Kaunti ya Meru walikutana na Rais Ruto katika ikulu ndogo ya Sagana ili kupata mawaidha yake kuhusu maridhiano.
“Tumekuja kwako kama baba wa Wameru kwa sababu nyumba yetu inateketea na hatuwezi kuangalia upande mwingine,” ikasema barua iliyowasilishwa kwa Rais kutoka kwa viongozi hao wa kidini na Njuri Ncheke.
Kwa mujibu Katibu Mkuu wa Njuri Ncheke Josephat Murangiri, Rais aliwapa wazee hao na viongozi wa kidini idhini ya kuwaunganisha wanasiasa wa kaunti hiyo.
Kati ya wanasiasa ambao walikuwa wafike kwenye kamati ya maridhiano yenye wazee 25 na maaskofu ni Gavana Mwangaza, aliyekuwa waziri wa kilimo Mithika Linturi, Naibu Gavana Isaac Mutuma na wabunge na madiwani wote wa kaunti hiyo.
Bi Mwangaza amekuwa haonani uso kwa macho na naibu wake huku madiwani 56 kati ya 69 wakiwa wanampinga.
“Rais alituamrisha tukutane na viongozi wote kusuluhisha masuala tata. Pia alisema tuwasilishe ripoti kwake ili aitekeleze,” akasema Bw Murangiri.
“Ripoti iko tayari baada ya kukutana na viongozi wote na tumetoa mapendekezo yetu kwa Rais Ruto baada ya kuwasikiza wote. Hatuwezi kuruhusu kaunti yetu isambaratike,” akaongeza.
Wiki jana, madiwani 10 walijiondoa katika mchakato wa kumtimua gavana wakisema ni vyema kamati ya upatanishi inayoongozwa na Njuri Ncheke na viongozi wa kidini ipewe muda wa kufanya kazi yake.