Njaa inavyosukuma kina mama, wasichana kwenye migodi hatari ya dhahabu
KUTOKANA na hali ngumu ya maisha nchini, kumeshuhudiwa vifo vingi vya akina mama wakati wakichimba dhahabu kwenye migodi katika Kaunti ya Pokot Magharibi.
Kulingana na mila za jamii ya Pokot, wanawake wako na jukumu la kutafutia na kulisha familia huku wanaume wakichunga mifugo.
Wakiwa na shoka, jembe, beleshi na mabaseni ya mabati wanaelekea kwenye mito ama maeneo ya migodi kusaka bidhaa hiyo.
Wao huchimba mashimo na wakiwa na watoto migongoni, hutembea mwendo mrefu na kuchomwa na jua kali.
Akina mama husukumwa kwenye migodi kutokana na hali ya umaskini na njaa kutokana na uzembe wa wanaume wao.
Ukosefu wa mvua umesababisha baa la njaa huku akina mama, watoto na wakongwe wakifanya kazi hiyo.
Hata hivyo, kazi hiyo imechangia wanawake wengi kuuawa na majangili ama kukufia kwenye migodi wakisaka dhahabu.
Wakati mwingine, hufunikwa na udongo huku wanaume wao wakiwa wanaota jua.
Ann Chepurai, mama wa watoto sita, mkazi wa eneo la Kases anasema kuwa yeye kutumia siku nzima mtoni na siku ya mwisho huuza dhahabu kwa wachuuzi kwa Sh200.
“Mimi husaka dhahabu sababu ya njaa, watoto hawana chakula. Mwaka jana hatukuvuna. Jua liliangamiza mazao,” alisema.
Bi Chepurai anasema kuwa kwa wiki moja yeye kupata Sh600 na yote ananunua chakula.
“Kazi hiyo ni ngumu. Unachimba mashimo na unaumwa na mgongo na kuchoka pakubwa,” anasema.
Anasema kuwa mabadiliko ya hali ya anga na wizi wa mifugo huharibu maisha ya wakazi.
Mary Chemsuto, mchimba dhahabu anasema kuwa wao hufanya kazi hiyo kwa makundi.
“Ni kazi ya kubahatisha. Tunategemea dhahabu kulisha, kuelimisha na kuvisha familia,” anasema.
Bi Chemusto anasema kuwa alianza kazi akiwa msichana mdogo lakini bado anaishi maisha ya uchochole.
Anapambana kuelimisha wanawe wawili ambao wako shule ya upili.
Anasema kuwa mamba na nyoka huwasumbua wakiwa kwenye mito.
Easter Chepukorio, mama wa miaka 45 anasimulia jinsi amekuwa aking’ang’ana kulisha wanawe nane huku mzee wake akishughulika na kuchunga mifugo.
“Nimefanya kazi hiyo kwa miaka kumi kulisha familia,” anasema.
Cheptoo Lotudo, msichana wa miaka 18 kutoka eneo la Alale ambaye aliponea kifo chupuchupu akisaka dhahabu na wenzake anasema kuwa alianza kazi hiyo akiwa na miaka nane.
“Sisi hufika hapa asabuhi na mapema na kufanya kazi siku nzima. Siku moja niliponea kifo chupuchupu baada ya kuangukiwa na udongo,” anasema.
Anasema kuwa kuna wachuuzi ambao huwanyanyasa kwa kununua bidhaa hiyo kwa bei ya chini.
Haya yanajiri baada ya akina mama wawili kuuawa na majangili wakisaka dhahabu katika kijiji cha Kases, eneo la Ombolion wiki jana.
Mwaka wa 2022, akina mama 3 walifunikwa kwenye migodi katika eneo la Kambi Karaya kwenye barabara kuu ya Kitale -Lodwar.
Msichana mwenye umri wa miaka 15, Nakiru Ngolenyang alifunukiwa na migodi kwenye kijiji cha Narworwo, Lokesheni ya Alale, kaunti ndogo ya Pokot Kaskazini. Mwaka huo huo, wanawake 3 walifunikwa wakichimba dhahabu katika kijiji cha Nyelnyel eneo la Ptokou.
Chifu wa Nasolot Michael Mwotot anasema kuwa mashimo ya dhahabu ni hatari.
Anasema kuwa akina mama wengi waliasi mashamba na kuanza kazi hiyo.