Kesi ya sakata ya NYS yaahirishwa hadi Januari 14
Na RICHARD MUNGUTI
KWA siku ya pili, kesi dhidi ya katibu mkuu katika Wizara ya Ugatuzi Bi Lillian Wanja Muthoni Mbogo Omollo na washukiwa wengine 32 wanaoshtakiwa kwa sakata ya ulaghai wa Sh60 milioni kutoka kwa shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) haikuendelea.
Mawakili wanaowatetea washukiwa hao 33 waliomba mahakama iwape muda wa siku tatu kusoma nakala za ushahidi katika kesi hiyo mpya.
“Tunaomba muda wa kusoma nakala za usahidi katika kesi hii mpya inayotokana na kuunganishwa na kesi tatu za sakata hii ya NYS,” alisema wakili Kirathe Wandugi.
Bw Wandugi na mawakili wengine walimweleza hakimu mwandamizi Bw Peter Ooko kuwa baadhi ya washtakiwa walisomewa mashtaka jana kwa mara ya kwanza na “ hawajakabidhiwa nakala za mashahidi.”
Akitoa uamuzi kuhusu ombi hilo hakimu alisema, “Sheria imewapa fursa washukiwa kujiandaa na kusoma nakala za ushahidi. Kwa ajili ya maslaha ya umma nitaahirisha kesi hii hadi Januari 14 kuwezesha mawakili na washtakiwa kujiandaa.”
Awali viongozi sita wa mashtaka walichelewa kufika kortini na kulazimisha kesi iahirishwe kuwasubiri.
Kiongozi wa mashtaka ni Bi Verah Amisi akisaidiwa na mawakili wengine watano wa Serikali.
Mnamo Jumatatu mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Noordin Haji aliwasilisha mashtaka 49 mapya dhidi ya washtakiwa.
Bi Omollo, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NYS Richard Ndubai , wafanyakazi waliosimamishwa kazi wa NYS na wafanya biashara Catherine Njeri Kamuyu, Sarah Murugu, Andrine Grace Nyambura Mbare, Antony Makara Wamiti na Peter Wagura Kimari walikanusha mashtaka mapya yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.
“Tumewasilisha mashtaka mapya dhidi ya washukiwa hawa katika kesi tatu zilizounganishwa na kuwa moja,” alisema kiongozi wa mashtaka Bi Verah Amisi.
Bi Amisi aliomba mashtaka yote dhidi ya washtakiwa yasomwe upya ndipo wajibu tena.
Bi Omollo, Bw Ndubai na wafanyakazi wa NYS waliosimamishwa kazi walikabiliwa na shtaka la kufanya njama za kuiba Serikali Sh60,598,800 kat ya Aprili 6 2016 na Aprili 27 2017.
Bi Omollo alikabiliwa na mashtaka sita ya kutumia mamlaka yake vibaya kwa kuamuru malipo ya Sh26,660,000 kwa Njeri, Murugu , Nyambura na kampuni yao ijulikanayo Ersatz Enterprises Limited.
Katibu huyo aliyesimamishwa kazi alikabiliwa na shtaka lingine la kulipa kimakosa kampuni ya Arkroad Holdings Limited Sh24,866,800.
Pia alishtakiwa kwa kulipa kampuni nyingine inayomilikiwa na Andrine Grace Nyambura Mburu ijulikanayo Kalabash Food Supplies Sh9,072,00
Wafanyabiashara hao walikana kuipora Serikali jumla ya Sh56,698,800 kwa njia ya undanganyifu.