Michezo

Arsenal waamini Calafiori atamaliza shida zao

Na JOHN ASHIHUNDU NA MASHIRIKA July 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

ARSENAL wanaamini Riccardo Calafiori aliyesajiliwa kutoka Bologna kwa Sh4.2 bilioni atamaliza matatizo yao katika safu ya kiungo ambayo imewasumbua kwa muda mrefu.

Klabu hiyo imekiri kwamba imekuwa ikitafuta mlinzi wa aina hiyo kwa muda mrefu.

Raia huyo wa Italia mwenye umri wa miaka 22 ni miongoni mwa wachezaji waliotoa mchango mkubwa kwa klabu ya Bologna ambayo ilifuzu kwa michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya kwa mara ya kwanza.

Calafiori alikuwa katika kikosi cha timu ya Italia kilichoshiriki fainali za Mataifa ya Ulaya (Euro 2024) nchini Ujerumani chini ya kocha Luciano Spalletti.

Anakumbukwa kwa kumuandalia Mattia Zaccagni pasi iliyochangia bao la ushindi ambalo lilisababisha kubanduliwa kwa Croatia katika hatua ya makundi.

Kuimarika kwa staa huyo kumewashangaza wengi hasa baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na jeraha baya kabla ya kurejea na kuanza kuhangaika kwa kutoka AS Roma hadi Genoa na baadaye Basel katika kipindi kisichozidi  miezi minane.

Kiwango chake kimekuwa cha kuvutia kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita kama beki wa katikati.

Calafiori ambaye amejiunga na kambi ya Arsenal katika jimbo la Los Angeles nchini Amerika alisajiliwa na Roma kama beki wa kushoto, huku akicheza pia kama mshambuliaji wa pembeni, kabla ya kuanza kuanza kusakata kama beki wa katikati.

Akiwa na Bologna msimu uliopita, Calafiori alifananishwa na John Stones anayechezea Manchester City na timu ya taifa ya Uingereza.