Habari Mseto

Bondi ya Kiislamu Linzi Sukuk yapata nafasi katika soko la hisa

Na LABAAN SHABAAN July 31st, 2024 2 min read

NI tukio la kihistoria Kenya baada ya bondi ya Sukuk kuingia katika soko la hisa Kenya kwa mara ya kwanza.

Sukuk ni bidhaa ya kifedha ya Kiislamu inayotolewa na serikali au mashirika kutafuta pesa kutoka kwa wawekezaji.

Hutolewa kwa muda ili kufadhili wawekezaji binafsi, biashara za mashirika au miradi ya serikali.

Mnamo Jumatano Julai 31, 2024, Rais William Ruto alizindua bondi ya kwanza inayofuata sheria za kiislamu.

Bondi hii almaarufu Linzi Sukuk, sasa imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE).

Hii ni baada ya Shirika la Linzi Finsco Trust kutuma maombi kwa Mamlaka ya Masoko ya Mtaji nchini (CMA) mwaka wa 2023.

“Ni tukio la kihistoria kuorodhesha bidhaa ya kwanza inayofuata sheria ya Kiislamu katika soko la hisa,” akasema Rais alipozindua Linzi Sukuk.

Mwenyekiti wa NSE Kiprono Kittony akasema “Soko la Hisa la Kenya limepanua wigo wa jukwaa la uwekezaji kwa umma kupitia kuorodhesha bidhaa hii.”

Uwekezaji huo wa Kiislamu wenye thamani ya Sh3 bilioni unalenga kufadhili miradi ya maendeleo.

Uislamu na Riba

Sukuk hufuata kanuni za Kiislamu za fedha zinazoepuka riba badala yake kuwezesha uzalishaji wa pesa kutoka kwa pesa.

Wawekezaji hupata faida kutoka kwa ushirikishaji wa mali katika biashara mbalimbali.

Mwalimu wa dini ya Kiislamu Ustadh Feiswal Omar, amefurahishwa na hatua hii ya serikali inayoendana na matakwa ya dini.

“Mungu amekataza desturi ya kutoza riba na anayejihusisha nayo atakuwa ametangaza vita na Mungu. Mwenye kula riba atapata hasra na ataingia moto wa jahanamu,” akaeleza Bw Feiswal, Ustadh wa msikiti wa Masjid Mariam, Githurai kaunti ya Kiambu.

Akinukuu aya moja ya msahafu wa Quran, Bw Feiswal amesema mlaji wa riba hujiondolea baraka maishani mwake.

“Ukitoa pesa kwa moyo, inafaa urejeshewe kiasi hicho hicho sababu ulaji riba ni haramu kwa Muislamu.”

Wawekezaji

Uzinduzi wa bondi ya Linzi Sukuk unatarajiwa kuvutia wawekezaji mbalimbali.

Watakaochangamkia nafasi hii ya kibishara kwa wingi ni wale wanaotafuta uwekezaji unaoheshimu kanuni za Kiislamu.

Serikali inalenga kutumia nafasi za bondi hii kufadhili ujenzi wa zaidi ya nyumba 3000 chini ya mpango wa makazi nafuu unaoendeshwa na serikali.