Habari Mseto

Bodaboda ‘kunyolewa’ jijini katika mipango mipya ya Sakaja

Na KEVIN CHERUIYOT August 1st, 2024 1 min read

SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi imeweka mikakati ya kudhibiti sekta ya bodaboda ambayo ni jukwaa la kibiashara na ajira kwa wafanyakazi wengi.

Afisa Mkuu wa Masuala ya Usalama, Tony Kimani Jumatano alisema kuwa kuna mipango ambayo kaunti imekuwa ikiendelea nayo ya kupunguza idadi ya wahudumu wa bodaboda katikati mwa jiji.

Bw Kimani alisema kaunti ina wahudumu wa bodaboda 700 ambao wamesajiliwa na wamekuwa wakihudumu katikati mwa jiji kila siku. Alisema idadi hiyo ni ya juu zaidi na si rahisi kudhibiti.

Aidha, idadi hiyo inaweza kuwa ya juu zaidi kwa sababu kuna wahudumu wa bodaboda ambao wanafanya kazi katikati mwa jiji kinyume cha sheria.

Afisa huyo aliongeza kuwa, kuna hatua ambazo zinahitajika kuhakikisha idadi ya wahudumu wa bodaboda inapungua hadi 300, malengo ambayo wameweka japo si rahisi kufikiwa.

“Kama serikali ya kaunti lazima tupunguze idadi ya wahudumu wa bodaboda katikati mwa jiji. Najua hiki ni kibarua kigumu lakini tutapambana na kuafikia kile ambacho tunakilenga,” akasema Bw Kimani.

Jinsi ilivyo kwa sasa, kaunti haina sheria au mwongozo ambao unadhibiti au kusimamia sekta ya uchukuzi wa bodaboda nchini.

Kaunti hata hivyo, imekanusha kuwa inawatimua wahudumu wa bodaboda jijini kutokana na wimbi la maandamano ambalo limekuwa likishuhudiwa nchini.

Pia, kaunti imesema kuna maafisa maalum ambao watakuwa wakisimamia sekta ya bodaboda na wanastahili kuwanyaka wale ambao wanaendeleza shughuli zao kinyume cha sheria.

“Si afisa yeyote katika serikali ya kaunti hasa katika idara ya usalama ataruhusiwa kumnyaka mhudumu wa bodaboda katikati mwa jiji. Kuna maafisa ambao wametengewa majukumu hayo katika barabara mbalimbali,” akaongeza Bw Kimani.

Bw Sakaja alipoingia mamlakani mnamo 2022, aliwaruhusu wahudumu wa bodaboda wafanye kazi katikati mwa jiji.