Habari Mseto

Visa vya wanandoa kuuana vyashtua wakazi wa kijiji cha Murkwijit

Na OSCAR KAKAI August 1st, 2024 2 min read

MAAFISA wa polisi katika mji wa Kapenguria wameanzisha msako kuhusu tukio ambalo mwanaume mmoja anadaiwa kumua mkewe kisha baadaye akajinyonga kwenye mzozo wa nyumbani.

Wakazi wa kijiji cha Cherelio, eneo la Murkwijit katika kaunti ya Pokot Magharibi waliamka kwa mshangao Jumanne asubuhi kwa tukio la kutisha ambapo mwanaume huyo alimuua mkewe kisha akajitoa uhai.

Benjamin Morogo Mutai, 53, alimkata koo mkewe, Teresa Chepkemoi, 47, kwenye mzozo mkubwa. Miili ya wawili hao ilipatikana na majirani ambao walishuku kulikuwa na shida kwenye boma hilo.

Naibu wa Kamanda wa kaunti ndogo ya Pokot Magharibi Richard Omanga alithibitisha mkasa huo akisema kuwa uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha tukio hilo.

“Ilifanyika kutokana na mzozo wa nyumbani ambao ulienea. Tunafanya uchunguzi kujua kilichofanyika,” alisema.

Bw Omanga alisema kuwa, “Mwanaume alimdunga kisu mkewe kwenye kifua kisha akaaga dunia. Baada ya kutekeleza tukio hilo alijinyongea ndani ya nyumba. Tunashtumu vikali tukio hilo,” alisema akiongeza kusema kuwa wawili hao wamekuwa na mzozo wa nyumbani kwa muda mrefu.

Wakazi wa eneo la Murkwijit wameachwa na mshangao na huzuni huku wengi wakitaka hamasisho kuhusu suala la kutatua mizozo ya nyumbani.

Mike Kiprop, mtu wa ukoo wa familia hiyo alisimulia tukio hilo:

“Tulifika kwa boma na kupata mwanamke bado anapumua nje ya nyumba. Alikuwa anavuja damu mwili wote. Inaonekana mwanaume alimvamia akiwa nje kisha akaingia kwa nyumba na kujinyonga.”

“Tulimpeleka mke kwa hospitali tukiwa na imani ya kupona lakini alifariki tukiwa njiani.”

Sammy Moran, jirani anasema kuwa familia hiyo imekuwa na mizozo ya mara kwa mara.

“Familia hiyo imekuwa na mizozo mingi ya nyumbani ambayo iliwapaleka kwenye kituo cha polisi kusuluhisha,” alisema.

Bw Moran alisema kuwa alikerwa na kushangazwa na tukio hilo.

“Siamini kilichotokea. Tulikuwa kwenye kituo cha polisi tukifikiria tumesuluhisha mizozo. Nilimpigia simu mwanaume ikiwa angerudi kwenye kituo cha polisi Jumanne kuendelea na mazungumzo lakini niliamkia masaibu,” anasema.

Alisema kuwa watu wa ukoo walikuwa wamezuiwa kuingilia mzozo huo ambao hasa ulihusu kuuza kwa maziwa na mahindi.

Miili ya Benjamin Morogo Mutai na Teresa Chepkemoi ilipelekwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kapenguria kufanyiwa uchunguzi.

Wakazi wanataka hamasisho kuhusu masuala ya ndoa kufanyika na kutatua mizozo ya ndoa.