Michezo

Kenya nusura ikamate mkia mbio za kupokezana vijiti Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE August 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KENYA imebanduliwa katika mbio za mseto za kupokezana vijiti za mita 400 kwenye Michezo ya Olimpiki baada ya timu ya David Sanayek, Veronica Mutua, Boniface Mweresa na Mercy Chebet kukamata nafasi ya saba jijini Paris, Ufaransa, Ijumaa.

Mchujo huu ulikuwa pia na washiriki kutoka Jamaica, Bahamas, Poland, Amerika, Ubelgiji, Ufaransa na Uswisi.

Boniface Mweresa aking’ang’ana kufikia wenzake upesi kuwapokeza kijiti katika mbio za mita 400 jijini Paris, Ufaransa. Picha|Joan Pereruan

Wakenya walimaliza mbele ya Bahamas pekee baada ya kukamilisha mbio hizo kwa dakika 3:13.13.

Waamerika wametinga fainali kwa kushinda mchujo huo kwa rekodi ya dunia ya 3:07.41 wakifuatiwa na Ufaransa (3:10.60) na Ubelgiji (3:10.74).

Waamerika walifuta rekodi yao ya dunia ya 3:13.20 waliyoweka mjini Eugene mwaka 2016.

Pia, walifuta rekodi ya Olimpiki ya 3:09.87 iliyowekwa na Poland katika makala ya 2020 mjini Tokyo, Japan.