HabariHabari za Kitaifa

Sikuuza JKIA, Murkomen anawa mikono

Na CHARLES WASONGA August 4th, 2024 2 min read

WAZIRI mteule wa Michezo na Masuala ya Vijana, Kipchumba Murkomen, amekana madai kuwa “aliuza” Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) katika mpango uliohusisha kampuni moja ya India.

Akijitetea mbele ya wabunge Jumamosi jioni mnamo Agosti 3, Bw Murkomen, ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi hadi Julai 11, 2021 alipofutwa kazi pamoja na wenzake 20, alisisitiza kuwa kama Waziri hana mamlaka ya kuuza au kukodi mali ya umma kwa kampuni ya kibinafsi kivyake.

“Sijatia saini mkataba na kampuni yoyote ili kuuza au kukodi JKIA. Sina uwezo na mamlaka ya kufanya hivyo chini ya mpango wa Ushirikiano kati ya Serikali na Kampuni za Kibinafsi (PPP). Kwa hivyo, sijauza JKIA kwa vyovyote,” Murkomen akaeleza kufuatia madai kuwa aliuza JKIA kwa Kampuni ya Adani Airport Holdings Ltd, kutoka India.

Alifichua kuwa kile anachoelewa ni kwamba kampuni hiyo imewasilisha ombi kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) ikitaka kuwekeza katika uwanja wa JKIA.

“Kampuni hiyo imetuma maombi na hiyo ni hatua ya kwanza. Na ni ombi la kukodisha sehemu ya JKIA sio kuinunua. Mchakato wa ukodishaji ni mrefu chini ya mpango wa PPP na sharti uhusishe maoni kutoka kwa Wakenya ambao ndio wamiliki halisi wa mali hiyo,” Bw Murkomen akasema alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uteuzi kupigwa msasa kuhusu ufaafu wake kushikilikia wadhifa wa Waziri wa Michezo.

Waziri huyo mteule alieleza kuwa mpango huo pia sharti uidhinishwe na baraza la mawaziri, hatua ambayo haijafikiwa ‘kwa sababu mahitaji ya kisheria hayatimizwa.’

“Kabla ya hati za mpango huo kufika mbele ya mawaziri, sharti uidhinishwe na Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Fedha. Kwa hivyo, ni wazi kwamba shughuli kama hii haiwezi kuendeshwa na mtu mmoja pekee; waziri wa uchukuzi,” Bw Murkomen akaeleza.

Suala la uuzaji au ukodishaji wa JKIA liliangaziwa hadharani kwa mara ya kwanza majuma mawili yaliyopita na Seneta wa Kisii Richard Onyonka.

Seneta huyo aliwasilisha malalamishi yake katika Bunge la Seneti akitaka maelezi kutoka kwa Wizara ya Uchukuzi kuhusu kile alichotaka kama “njama fiche ya kuuzwa kwa JKIA kwa kampuni ya Adani ya India.”