KAULI YA WALIBORA: Yamezuka mapuuza kwa fasihi zetu zinazosheheni umilisi usiopitwa na muda
NA PROF KEN WALIBORA
Katika utangulizi wa kitabu chake Swahili Sayings, S. S. Farsi anasema kwamba kipera cha fasihi simulizi kiitwacho vitendawili kilikuwa katika hatari ya kuangamia kutokana na kutoweka kwa wazee.
Farsi alikuwa mzawa wa Zanzibar kama anavyotaja katika utangulizi huo, elimu ya Magharibi ilikuwa imeingia kwao na kuiweka fasihi simulizi katika hatari ya kuangamia. Anaendelea kusema kwamba:
“Kwa muda kati ya magharibi na wa kulala (watoto) walikaa ndani wakifurahiwa kuwasikiliza wanawake wazee wakiwatolea vitendawili na kuwasimulia hadithi. Hadithi hizi siku zote zilikuwa na kusudi katika mafundisho ya adili na elimu.”
Kile anachomaanisha Farsi ni kwamba sanaa ya vitendawili na hadithi za wazee ilikuwa imekitwa katika mfumo asilia wa elimu ya kuadilisha. Yaani zilielimisha na kuadilisha. Elimu na adili vilikwenda sambamba kama watoto pacha.
Kabla ya elimu ya kisasa Wafrika walimu na elimu yao, labda yenye msingi wa umilisi kuliko ile tunayosukumiziwa. Kumbe Wafrika tangu hapo wamekuwa na hazina yao ya kutwaa maarifa na maadili na mafundisho ili kuchuana na mawimbi na masaibu ya maisha.
Kwa kuhofia kwamba hazina hizi zitapotea na kutokomea kama moshi, Farsi alikusanya vitendawili, desturi, na methali za Waswahili wa Unguja. Anasema Farsi: “Kusudi la vitabu hivi ni kuandika baadhi ya desturi hizo na mapokeo kabla hayajasahauliwa kabisa.” Kauli hizo kaziandika miongo mingi iliyopita.
Vitabu vyake nilikumbana navyo nilipokuwa shule ya upili miaka mingi iliyopita, nao watangulizi wangu wao walivipata kuko huko, vimeshatumiwa na watangulizi wao. Ila twauliza: Je, hofu yake Farsi ilikuwa na msingi wa dhati.
Hebu wazia niliyoyaona katika kongomano la fasihi simulizi lililofanyika katika hoteli ya kifahari ya Leisure Lodge, Diani mwaka 2010. Nilisafiri toka Marekani kuja kuhudhuria kongomano hili kubwa sana la kimataifa kuhusu fasihi simulizi.
Hapo ndipo nilipokutana kwa mara ya kwanza na mbishi mmoja raia wa Sudan, aitwaye Taban Li Lyong, msomi aliyejaa taraghani. Ila hayo ya takaburi yake tuyazungumze siku nyingine. Tulenge mazungumzo niliyokuwa nayo na mhadhiri mmoja wa fasihi kutoka Uganda.
Mhadhiri huyo sikumbuki jina ila alichokisema kinashtua mpaka leo. Alisema kwamba anaamini kabisa kwamba fasihi simulizi ya Kiafrika haina umuhimu wowote.
Kuishughulikia kwa utafiti, ufundishaji na ufundishwaji ni kupoteza muda, alishikilia kani. Niliemewa. Nilipomuuliza kama hivyo ndivyo anavyowafundisha wanafunzi wake wa fasihi chuoni kule Uganda, akajibu kwa kujiamini, “Ndivyo.” Kwa makadirio yangu, taraghani au takaburi yake ama ilishabihiana na ya Taban Li Lyong, au iliizidi.
Walau Taban yeye anaheshimu kidogo dafina ya fasihi simulizi ya Kiafrika na ameandika vitabu na makala kuhusu masuala haya.
Kwa upande wake mhadhiri wa Uganda aliamini fasihi simulizi, ni ovyo, bure kabisa. Anathibitisha hofu ya Farsi kwama labda yatazuka na sasa yamezuka mapuuza kwa fasihi zetu zinazosheheni umilisi usiopitwa na wakati.