Lamu haina Mahakama Kuu licha ya ahadi ya Koome 2023
SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imejitenga na kucheleweshwa kwa ujenzi wa mradi wa Mahakama Kuu eneo hilo.
Aprili 2023, Jaji Mkuu (CJ), Martha Koome alifika Lamu ambapo alikabidhiwa hatimiliki za ardhi mbili na Gavana wa Lamu, Issa Timamy.
Ardhi hizo zilinuiwa kujengwa Mahakama Kuu eneo la Mokowe na kisha nyumba za wafanyakazi wa mahakama hiyo eneo la Hindi, Lamu Magharibi.
Wakati wa hafla hiyo, CJ Koome aliahidi kwamba ujenzi wa mahakama hiyo kuu ungeanzishwa mara moja.
Mwaka mmoja unusu baadaye, ujenzi wa mahakama hiyo kuu haujazinduliwa huku ardhi zilizotolewa zikisheheni magugu.
Katika mahojiano na Taifa Dijitali Jumatatu, Agosti 5, 2024, Katibu wa Serikali ya Kaunti ya Lamu, Bw Ali Abbas alisema wao walishatekeleza jukumu lao la kupeana ardhi kwa idara ya mahakama na kwamba jukumu la ujenzi wa mahakama husika liko kwa serikali kuu.
“Kama kaunti, jukumu letu lilikuwa ni kukabidhi ardhi kwa mahakama na tumefanya hilo kitambo. Kuhusu ni lini ujenzi wa mahakama utaanza, hilo halituhusu. Cha msingi ni kuwa ardhi ipo ilishakabidhiwa wahusika,” akasema Bw Abbas.
Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Dijitali walisisitiza haja ya mradi huo kuharakishwa ili kuwapunguzia gharama ya kusafiri nje ya Lamu kupata huduma za mahakama kuu.
“Lamu hakuna mahakama kuu. Inatulazimu kusafiri hadi Garsen kaunti ya Tana River, Malindi na Mombasa tunapokuwa na kesi zinazoshughulikiwa na mahakama kuu. Tukiwa na mahakama yetu kuu hapa Lamu hizi gharama zitapungua,” akasema Bi Husna Alwy.
Bw Ahmed Abdalla alitaja Lamu kuwa kaunti inayohitaji huduma za haraka za mahakama kuu.
Kulingana na Bw Abdalla, Lamu imekumbwa na visa vingi vya kigaidi miaka ya awali, hali ambayo imeacha vijana wengi wakishikwa, kupotezwa ilhali wengine wakisafirishwa nje ya Lamu kufikishwa kwenye mahakama kuu.