Ruto aliniomba usaidizi, nikampa, Raila aambia Wakenya
KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga kwa mara ya kwanza ameitetea serikali inayoshirikisha wanachama wa upinzani baada ya Wakenya kumkosoa Rais William Ruto kwa kuteua viongozi watano wa ODM katika baraza lake la mawaziri.
Akiongea jana katika eneo bunge la Kibra, Nairobi, Bw Odinga alisema utawala wa Kenya Kwanza ulimwomba usaidie kuleta utulivu nchini kufuatia msururu wa maandamano ya kuupinga uliofanywa na vijana wa Gen Z.
“Walikuwa wamelemewa ndiposa wakavunja baraza la mawaziri. Wakatuomba usaidizi. Na tukakubali kuwapa wataalamu. Sasa mtaona mambo yakibadilika,” Bw Odinga akasema.
Alikuwa akirejelea mawaziri watano wateule ambao juzi walipendekezwa na Rais Ruto kushikilia nyadhifa mbalimbali za uwaziri.
Wao ni pamoja na aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya aliyependekezwa kuwa Waziri wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika, aliyekuwa Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho aliyendekezwa kuwa Waziri wa Uchumi wa Majini, Uchumbaji na Masuala ya Majini, Opiyo Wandayi aliyependekezwa kuwa Waziri wa Kawi na Bidhaa za Petroli na John Mbadi aliyependekezwa kuwa Waziri wa Fedha.
Mwingine ni mwanachama wa Kamati ya Kusimamia Uchaguzi katika ODM Beatrice Askul Moe aliyependekezwa kuwa Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda.
Akiwahutubia wafanyabiashara waliathiriwa na mkasa wa moto ulioteketeza mali yao katika Soko la wazi la Toi, Bw Odinga aliamuru ua la saruji ujengwe kulizunguka soko hilo.
“Namwamuru Gavana Sakaja (Johnson) kuanzisha mara moja ujenzi wa ua na soko la kisasa hapa. Serikali inazo pesa za kuanzisha ujenzi huu ili wale ambao wamekuwa wakipania kunyakua ardhi hii waambulie patupu,” Bw Odinga akasema.
Kiongozi huyo wa upinzani alieleza kuwa kwa miongo mitatu iliyopita, amekuwa akipambana na wanyakuzi wa ardhi ambao walitaka kutwa Soko la Toi wakisaidiwa na maafisa fulani wa Wizara ya Ardhi.
“Nipigania wafanyabiashara hawa kwa miaka 30 sasa. Nataka kusema kuwa hawatafaulu kunyakua kipande hiki cha ardhi. Wanyakuzi hao wanataka kuchukua nafasi, kujigawanya kisha wajenge nyumbani. Mara nyingi wao huenda katika Afisi ya Ardhi kuvuruga rekodi.” Bw Odinga akaeleza.
Aliamuru kwamba Sh100 milioni ambazo Bunge la Kaunti ya Nairobi ilitenga kufadhili ujenzi wa vibanda vya kisasa katika Soko la Toi zinapasa kuanza kutumika mara moja.
Bw Odinga alitoa msaada wa Sh1.5 milioni, pesa taslim, kuwasaidia wale walioathirika katika mkasa huo wa moto. Aidha, alitoa mabati 1000 za ujenzi wa vibanda vipya vitakavyotumiwa na wafanyabiashara kabla ya ujenzi wa soko jipya kuanza.
Kwa upande wake, Seneta wa Nairobi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alitoa Sh250,000 huku Mbunge wa Kibra Peter Orero akatoa vifaa vya ujenzi
Tafsiri: Charles Wasonga