Ufaransa kuvaana na Uhispania fainali ya soka Olimpiki
PARIS, Ufaransa
TIMU ya taifa ya Ufaransa itakutana na Uhispania siku ya Ijumaa jioni ugani Parc des Princes kwenye mechi ya fainali ya kuwania ubingwa wa taji la Olimpiki, huku Misri wakipambana na Morocco, Alhamisi jioni kwenye ya mechi ya kutafuta mshindi wa nishani ya Shaba.
Kikosi hicho cha kocha Thierry Henry kilifuzu baada ya kuibandua Misri kwa 3-1 katika nusu-fainali iliyochezewa Groupama Stadium (Parc Olympique Lyonnais), usiku wa kuamkia leo.
Jean-Philippe Mateta alifungia wenyeji mabao mawili huku Michael Olise akiongeza la tatu.
Misri walitangulia kupata bao kupitia kwa Mohamoud Saber.
Uhispania walifaulu baada ya kubandua Morocco 2-1 katika nusu-fainali iliyochezewa Stade de Marseille jijini Lyon.
Morocco waliongoza kwa 1-0 lililofungwa mapema na Soufiane Rahimi kupitia mkwaju wa penalti, kabla ya Uhispania kutoka na nyuma na kupata mabao ya ushindi kupitia kwa Juanlu Sanchez na Abel Ruiz.