25/06/2019

Wambora akabiliana na wimbi jipya la kumtimua

Na GEORGE MUNENE

HUENDA Gavana wa Embu, Martin Wambora akakabiliwa na hoja nyingine ya kumwondoa afisini ikiwa madiwani (MCAs) wa kaunti hiyo watatekeleza tishio lao jipya.

Viongozi hao wanalalamika kuwa maendeleo yamekwama katika kaunti hiyo huku Gavana Wambora akidinda kuitisha mkutano wa viongozi ili kujadili kile wanachodai ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa “mwendo wa kinyonga.”

Walidai kuwa miradi kama ujenzi wa madaraja na barabara ambao unapaswa kuwa wa manufaa makubwa kwa wananchi umekwama ilhali Gavana Wambora hafanyi lolote kuikwamua.

“Ujenzi wa madaraja ya Kwangochi na Kigumo umekwama huku barabara ya kutoka Mukenyu kwenda Kathangari inayopitia maeneo yenye utajiri mkubwa wa kilimo iko katika hali mbaya,” akasema diwani wa wadi ya Ruguru- Ngandori, Bw Muturi Mwambo.

Madiwani hao walilalamika kuwa hali ni mbaya katika kaunti hiyo na wakamtaka Bw Wambora kuitisha mkutano wa kujadili masuala ya maendeleo katika kaunti ya Embu, la sivyo aondolewe mamlakani. Walitoa makataa ya siku saba kwa Bw Wambora kuandaa mkutano wa viongozi la sivyo wawasilishe hoja ya kumwondoa mamlakani.

“Nitadhamini hoja ya kumwondoa mamlakani gavana Wambora ikiwa hataheshimu wito wetu kama madiwani wa kutaka akutane nasi ili tujadili masuala ya maendeleo. Tumekasirishwa na kukwama kwa miradi mingi ya maendeleo,” akasema Bw Mwambo.

Naye diwani wa Kithimu Bw Michael Njeru alisema, Gavana Wambora amelemewa na kundi la watu fulani wenye nia mbaya na ambao wanamzuia kukutana na viongozi waliochaguliwa.

Kwa upande wake diwani wa Mbeti Kaskazini Peter Muriithi alionya huenda Gavana Wambora akakabiliwa na changamoto zilizomkabili 2013 ikiwa hataheshimu matakwa ya madiwani.

“Tutatumia mjeledi tuliotumia mnamo 2013 kumwondoa Gavana Wambora afisini,” akaongeza Bw Muriithi.

Akiongea katika kijiji cha Muthatari kitongojini mwa mji wa Embu wakati wa mazishi ya mwanaharakati wa Jubilee Wachira Ngiri, diwani huyo pia alilalamika kuwa sekta ya afya imeathirika vibaya kwa ukosefu wa dawa katika mazahanati.

Vile vile, MCAs hao walidai kuwa Sh50 milioni zilizotengwa kufadhili ukarabati wa Uwanja wa Michezo wa Embu zimeelekezwa kujenga kituo cha kukuza talanta na uwanja wa michezo wa Runyenjes.

Habari zinazohusiana na hii

Leave a Reply