• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Kiruka njia atoweka na long’i ya kalameni

Kiruka njia atoweka na long’i ya kalameni

Na SAMMY WAWERU

NYERI MJINI

Wakazi wa mji huu majuzi walitazama sinema ya bure kahaba alipotokomea na long’i ya jombi kwa kushindwa kulipia huduma za uroda lojing’i.

Baada ya kazi majira ya jioni, jamaa alipitia katika kilabu kimoja ambacho vipusa wanaofanya biashara ya ukahaba hufurika kwa wingi.

Inasemekana polo alipepesa macho yake na kufurahishwa na mwanadada mmoja na wakaanza gumzo. Baada ya mazungumzo, waliafikiana na akalipia lojing’i wakaingia ili aweze kuhudumiwa.

Dakika 30 baadaye, malumbano yalianza, kimwana alisikika akilalamika kwamba jamaa alikuwa amemhadaa. “Unadhani ni wanaume nimekosa wa kunilipa bora kuliko wewe?

Hebu wekelea Sh2,000 kwenye kiganja cha mkono wangu kama tulivyoagana, la sivyo utajua hujui,” aliwaka kidosho.

Kulingana na mdokezi, kalameni alikuwa amesalia na Sh500 pekee baada ya kulipa kodi ya lojing’i.

“Ninakuomba kwa unyenyekevu uniruhusu niende nifikapo kwangu nitakutumia hela kwa simu yako,” polo alijitetea. Kimwana hakumpa sikio hata kidogo, na kwa ghadhabu alichukua long’i ya jamaa.

“Sikuja mjini kutazama na kuharibu wakati na wanaume kama wewe,” kipusa alimfokea na kuondoka. Duru zinasema wahudumu wa lojing’i nao walichemka wakidai muda waliokuwa wamekodi chumba ulikuwa umeisha.

“Jamaa hakuwa na budi ila kuondoka akivalia boxer pekee,” alisimulia mdaku wetu. Watu waliacha gange zao na kumiminika kutazama jombi akitembea akiwa nusu uchi, baadhi yao wakimcheka na kumkejeli kwa kutamani asali bila uwezo wa kuigharamia.

Mama mmoja na ambaye ni msamaria mwema aliyemtazama akihangaika alitoa kanga kwenye kibeti na kumrushia.

Kalameni alifyatuka kama risasi, akiacha watu wakiangua kicheko.

 

You can share this post!

Wambora akabiliana na wimbi jipya la kumtimua

Gwiji wa ngwenje Jeff Bezos na mkewe kutalikiana

adminleo