Makala

Ruto alivyotumia njaa ya Raila kwa kiti cha AUC kumshawishi amkinge dhidi ya Gen Z

Na BENSON MATHEKA August 8th, 2024 2 min read

RAIS William Ruto alitumia azma ya uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) ya kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, kama mtego hadi akakubali chama chake kushirikiana na serikali kisiasa.

Wachambuzi wa siasa wanasema kwamba Bw Raila hakufaulu kujinasua kwenye mtego wa Rais Ruto kwa kuwa anataka kuungwa mkono na serikali katika azma yake ya kugombea wadhifa huo wa Bara.

Kiongozi wa chama cha Narc Kenya, Bi Martha Karua anasema Bw Odinga aliangukia mtego na hila za kisiasa alizowekewa kijanja na Rais Ruto.

Kulingana na Bi Karua, Bw Raila alijiondoa katika siasa za upinzani ili kuzingatia kampeni yake ya uenyekiti wa AUC ambayo anahitaji kuungwa mkono na serikali ya Kenya.

“Raila alijiondoa katika siasa za upinzani ili kufanya kampeni zake za kuwania kiti cha AU ambacho anahitaji Kenya Kwanza ndipo akipate.

Ni lazima apendekezwe na serikali ya Kenya na nadhani hapa ndipo mtego ulipomnasa na unaweza kuona wakati wa kuingia serikalini ni ule ambao stakabadhi zake ziliwasilishwa rasmi,” Bi Karua alisema kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio hivi majuzi.

Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, amejitangaza kuwa kiongozi wa muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja-One Kenya huku Bw Raila akiendelea na kampeni zake za kugombea wadhifa wa Bara.

Bi Karua anasema kuwa Bw Raila hana budi kuunga serikali iwapo anataka azma yake ya kiti cha AU ifaulu.

Hapa, kulingana na Bi Karua, ndipo mtego ulipotegwa na Rais Ruto.

Katika tukio ambalo Rais Ruto alitaja kama serikali jumuishi, kiongozi huyo wa Azimio alitoa baadhi ya viongozi wa ODM kuteuliwa katika Baraza la Mawaziri la serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Ruto aliteua manaibu viongozi wa ODM, Ali Hassan Joho, Wycliffe Oparanya, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi na mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho John Mbadi.

Bi Karua aliondoa chama chake katika muungano wa Azimio kufuatia hatua ya ODM kujiunga na serikali. Katika hafla zaidi ya moja, Bw Raila alikanusha makubaliano ya aina yoyote na Rais Ruto.

Hata hivyo, mnamo Jumatatu, waziri huyo mkuu wa zamani alipokuwa akizungumza katika Soko la Toi, Nairobi, alidai kuwa Rais Ruto aliomba msaada kutoka kwake ili kukomesha vuguvugu la Gen-Z ambalo lilikuwa likitishia kupindua serikali yake.

“Uliona wamelemewa na kazi, wakawafuta kazi waziri, wakaja kwetu wakiomba watu. Walikuja wakipiga magoti wakiomba tuwachangie baadhi ya watu,” Raila alifichua.

Kulingana na mchambuzi wa siasa, Dkt Isaac Gichuki, Bw Raila alijipata katika mtego asioweza kujinasua kwa kutaka serikali iidhinishe azma yake ya kugombea uenyekiti wa AUC.

“Kile ambacho Bw Raila na Ruto hawawezi kukiri ni kwamba kila mmoja alihitaji mwingine. Raila alihitaji Ruto zaidi katika azma yake ya AUC naye Ruto alihitaji Raila amsaidie kuokoa serikali yake iliyotishiwa na maandamano ya vijana,” akasema.