Habari za Kitaifa

Moses Kuria: Sina kazi sasa kwa sababu ya Gachagua

Na ERIC MATARA August 9th, 2024 2 min read

ALIYEKUWA Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria amemlamu Naibu Rais Rigathi Gachagua akisema ndiye aliyesababisha afutwe kazi pamoja na mawaziri wengine kutoka Mlima Kenya mwezi uliopita.

Bw Kuria alikuwa kati ya mawaziri waliotimuliwa na Rais William Ruto mnamo Julai wakati wa kilele cha maandamano yaliyokuwa yakiendelezwa na Gen Z nchini.

Pia, hakuwa na bahati kwa sababu alikuwa kati ya wale ambao hawakurejea kwenye baraza jipya la mawaziri lililotangazwa na Rais, japo lilijumuisha wandani wa kinara wa upinzani Raila Odinga.

Nafasi ya Bw Kuria imechukuliwa na Justin Muturi aliyekuwa kati ya mawaziri 19 walioapishwa Alhamisi katika Ikulu ya Nairobi. Bw Muturi alihudumu hapo awali kama Mwanasheria Mkuu.

Bw Kuria amelalamika kuwa sasa hana kazi kutokana na uhasama uliokuwa kati yake na Naibu Rais ambaye alimpiga vita alipokuwa akihudumu kama waziri.

“Kabla ya Rais Ruto kutekeleza mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri, Bw Gachagua alikuwa akitukashifu hadharani sisi tuliotoka Mlima Kenya. Hivyo ndivyo tuliishia kuondolewa serikalini,” akasema Bw Kuria.

Alikuwa akizungumza Jumatano eneo la Subukia, Kaunti ya Nakuru wakati wa mazishi ya mtangazaji nguli Prof Ngugi Njoroge.

“Kwa sasa sina kazi kwa sababu ya Gachagua. Wakati wa mabadiliko kwenye baraza la mawaziri, ODM iliwaleta wanasiasa vigogo kama vile Hassan Joho, Wycliffe Oparanya, John Mbadi. Lakini kutoka eneo letu wameteuliwa mawaziri watu limbukeni ambao hata kuhitimu kwao hakujulikani. Hata ukisaka maelezo kuwahusu hupati chochote,” akaongeza.

Bw Kuria anadai kiini kikuu cha Rais kuanzisha ushirikiano na Bw Odinga ni Bw Gachagua ambaye amekuwa akimpiga vita kutokana na ubabe wa siasa za Mlima Kenya.

Aidha, alisema Naibu Rais aliwateua wanasiasa wasiokuwa na uzoefu kutoka Mlima Kenya kwa sababu anaogopa ushindani kutoka kwa waliokuwa naye kwenye baraza la awali la mawaziri.

“Vita na uhasama wa kisiasa kati ya viongozi wa Mlima Kenya ndio ulisababisha mabadiliko kwenye baraza la mawaziri na wandani wa Raila waingie serikalini. Tulijikaanga wenyewe,” akasema.

Aliongeza kuwa eneo la Mlima Kenya limejipata pabaya kutokana na kukosa kuwa na chama chao cha kisiasa. Bw Kuria anasema alimfahamisha Bw Gachagua kuhusu hilo lakini hakumsikiliza.

“Sasa tumejipata kwenye shimo. Huwa nawaambia watu kuwa huwezi kuabiri gari la bwana harusi wakati wa harusi kwa sababu wakati wowote anaweza kukuitisha ufunguo na utatembea ukirejea nyumbani,” akasema Bw Kuria.

Licha ya uhasama wake na Naibu Rais, mbunge huyo wa zamani wa Gatundu Kusini alisema kuwa hawezi kuunga mkono hoja ya kumtimua Bw Gachagua ambayo inadaiwa baadhi ya wanasiasa wanapanga kuwasilisha bungeni.

“Tumejifunza. Kwa sasa sina shida wala siwezi kulipiza mabaya kwa mabaya kwa walionikosea akiwemo Naibu Rais. Siwezi kukubali jaribio lolote la kumng’oa Gachagua kama niko hai,” akasema Bw Kuria.

Kando na Bw Kuria, Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri amekuwa kati ya wanasiasa ambao wamemlamu naibu rais kutokana na kuingizwa kwa wandani wa Raila serikalini.