Habari Mseto

Wanaume watatu watupwa jela kwa ‘kuosha’ wanariadha

Na TITUS OMINDE August 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MISAKO mikali inayofanywa na Shirika la Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kututumua Misuli (ADAK) miongoni mwa wanariadha nchini inaendelea kuzaa matunda baada ya mahakama ya Eldoret kuwahukumu wanaume watatu waliopatikana na hatia ya kujifanya wafanyakazi shirika hilo na kuwalaghai wanariadha zaidi ya Sh800,000.

Mnamo Jumanne, watatu hao Thomas Kipyatich Kiptoo, Amos Mutai na Samuel Rono walihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na faini mbadala ya Sh30,000 kila mmoja.

Hakimu Mkuu wa Eldoret Dennis Mikoyan aliwahukumu washtakiwa baada ya miaka mitatu ya kuendesha kesi dhidi yao.

Mwendesha mashtaka aliambia mahakama kuwa washtakiwa walijiwasilisha kwa uwongo kama maafisa wa ADAK kwa nia ya kumlaghai mwanariadha Paul Kipchumba Lonyangata katika tarehe tofauti kati ya Septemba na Oktoba 2021 katika mji wa Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Bw Kiptoo pia alishtakiwa kwa shtaka lingine la kujiwasilisha kwa uwongo kama afisa wa ADAK kwa mwanariadha Purity Jebichii Changwony.

Mahakama iliambiwa kuwa watatu hao wanasemekana kujipatia jumla ya Sh776, 700 kutoka kwa wanariadha hao kati ya Septemba 2021 na Juni 2022.

Katika shtaka la pili, Bw Kiptoo alishtakiwa kwa kujipatia pesa kwa njia ya uwongo ambapo alidaiwa kujipatia Sh546,700 kutoka kwa Lonyangata kwa ahadi ya kumsaidia kusitisha kesi ya utumiaji wa dawa za kututumua misuli iliyokuwa ikimkabili kufuatia kutimuliwa kushiriki mashindano ya raidha na ADAK mnamo Februari 12, 2022.

Kulingana na stakabadhi zilizopo mahakamani, Bw Kiptoo alipokea pesa hizo kutoka kwa Lonyangata kati ya Oktoba 3 na Oktoba 31, 2021 huku mwandani wake, Bw Mutai, akiaminika kupokea Sh30,000 kutoka kwa mwanariadha huyo mnamo Oktoba 23, 2021.