HabariHabari za Kitaifa

Historia Beatrice Chebet akizoa dhahabu ya 10,000m Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE August 9th, 2024 2 min read

BINGWA mpya wa mbio za mita 5,000m Olimpiki, Beatrice Chebet, ameandikisha historia kwa kuwa wa kwanza kushindia Kenya dhahabu ya wanawake ya 10,000m kwenye michezo hiyo jijini Paris, Ufaransa, Ijumaa usiku.

Chebet, ambaye anajivunia kushikilia rekodi ya dunia ya 10,000 (dakika 28:54.14), aliongeza gia mita 150 za mwisho na kisha kufyatuka kama mshale zikisalia mita chache akielekea kuzoa ushindi kwa dakika 30:43.25.

Sasa amekuwa mwanamke wa kwanza kushinda 5,000m na 10,000m katika makala moja ya Olimpiki tangu Muethiopia Tirunesh Dibaba mwaka 2008.

Isitoshe, ni dhahabu ya kwanza ya Kenya katika 10,000m tangu kitengo hicho cha kinadada kijumuishwe kwenye Olimpiki kwa mara ya kwanza kabisa mnamo 1988 jijini Seoul, Korea Kusini.

Ni matokeo mazuri kwa timu ya Kenya ikizingatiwa kuwa kinadada wa Kenya wamekuwa wakioneshwa kivumbi huku makala ya hivi punde ya 2020 jijini Tokyo, Japan, yakiishia kwa Hellen Obiri, Irene Cheptai na Sheila Chelangat kukamata nafasi ya nne, sita na 16 mtawalia. Obiri anashiriki marathon pekee katika Olimpiki za wakati huu jijini Paris.

Chebet akimaliza wa kwanza mbio hizo za 10,000m Ijumaa. PICHA | REUTERS

Katika fainali ya Ijumaa, uongozi ulibadilishwa mara kadhaa kutoka kwa Rino Goshima (Japan), Rahel Daniel (Eritrea), Daisy Jepkemei (Kazakhstan), Lauren Ryan (Australia), Margaret Chelimo (Kenya), Fotyen Tesfay (Ethiopia) na Lilian Kasait (Kenya) kabla ya Chebet kutwaa usukani katika mita 70 za mwisho hadi kuzoa ushindi.

Mwitaliano Nadia Battocletti (30:43.35) na bingwa mtetezi Sifan Hassan (30:44.12) waliridhika na fedha na shaba mtawalia. Chelimo (30:44.58) na Kasait (30:45.04) walifunga tano-bora huku mahasimu wakuu wa Kenya, Ethiopia, wakiambulia pakavu tena.

Kenya sasa imepata medali katika mizunguko hiyo 25 kupitia kwa Chebet (dhahabu 2024 mjini Paris), Linet Masai (2008 mjini Beijing nchini Uchina (shaba), na Sally Kipyego (fedha) na Vivian Cheruiyot (shaba) mwaka 2012 mjini London nchini Uingereza. Cheruiyot pia alinyakua fedha mwaka 2016 mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Muethiopia Almaz Ayana anashikilia rekodi ya Olimpiki baada ya kushinda 10,000m kwa 29:17.45 mwaka 2016.

Kenya sasa imezoa medali sita baada ya Chebet kupata dhahabu ya 5,000m, Faith Kipyegon shaba ya 5,000m nao Mary Moraa (800m), Faith Cherotich (3,000m kuruka viunzi na maji) na Abraham Kibiwot (3,000m kuruka viunzi na maji) wakavuna shaba. Imeruka kutoka nafasi ya 31 hadi 24 baada ya dhahabu ya pili ya Chebet.