Makala

Presha ya Gen Z yapungua, yamfungua Ruto kusafiri

Na CHARLES WASONGA August 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KUFIFIA kwa presha ya maandamano ya vijana wa Gen Z, kuundwa kwa ‘serikali ya umoja wa kitaifa’ na kupungua kwa mivutano ndani ya muungano wa Kenya Kwanza, kunaonekana kumpa nafasi Rais William Ruto kuanza ziara za nje ya Kenya.

Mnamo Jumapili Agosti 11, 2024, Rais alizuru Rwanda ambako alihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa nchi hiyo Paul Kagame.

“Rais William Ruto anasafiri kuelekea Kigali, Rwanda kwa mwaliko wa Mheshimiwa Paul Kagame kuhudhuria kuapishwa kwake ili ahudumu kwa muhula wa nne afisini. Hii ni kufuatia ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa Julai 15,” Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed  alisema  kwenye taarifa fupi kupitia mtandao wa kijamii wa X.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa karibu miezi miwili kwa Dkt Ruto kuondoka nchini tangu vijana wa kizazi cha Gen Z walipoanzisha msururu wa maandamano kupinga sera za serikali yake.

Maandamano hayo yalianza Juni 18, 2024 kupinga Mswada wa Fedha wa 2024, ambao hatimaye Rais Ruto alikubali kuutupilia mbali.

Baadaye, vijana hao waliendeleza maandamano kushinikiza kujiuzulu kwa Dkt Ruto na serikali yake.

Walidai aliruhusu kukithiri kwa ufisadi na mwenendo wa mawaziri kupuuza matakwa ya wananchi huku wakiweka wazi maisha yao ya anasa yaliyoonekana kutumia vibaya mali ya umma.

Aliwatimua mawaziri

Hii ndio maana mnamo Julai 11 mwaka wa 2024, Rais aliwafuta kazi mawaziri wote 21, isipokuwa Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi, katika kile kilichoonekana kama hatua ya kutimiza matakwa ya Gen Z.

Majuma mawili baadaye, Dkt Ruto alifanya uteuzi wa mawaziri wapya, japo akawarejesha 11 miongozi mwa wale aliowapiga kalamu.

Aidha, aliteua viongozi wanne wa ODM katika baraza lake jipya la mawaziri kusudi kuunda kile alichokitaja kama serikali ya umoja wa kitaifa.

Wao ni; waliokuwa manaibu wa kiongozi wa chama hicho Wycliffe Oparanya na Hassan Ali Joho, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi na aliyekuwa kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa James Opiyo Wandayi.

“Nimeshirikisha viongozi wa upinzani ndani ya serikali kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila mtu anahisi kuwa sehemu ya serikali ili kwa pamoja tuweze kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na vijana wetu wa Gen Z,” Rais Ruto baada ya kuteua wanne hao kushikilia wizara za Vyama vya Ushirika, Uchumi wa Maji, Fedha na Kawi, mtawalia.

Uteuzi wa wanne hao uliibua msisimko mpya katika ngome za chama cha ODM Pwani, Magharibi mwa Kenya na Nyanza huku raia na viongozi wa maeneo hayo wakimsifu Dkt Ruto kwa kitendo hicho.

Ruto alivyotuliza Gen Z

Kulingana na Profesa Karuti Kanyinga hali hiyo ndiyo ilichangia kutoshuhudiwa kwa maandamamo “Nane Nane March” katika ngome hizo za kisiasa za kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Bila shaka uteuzi wa viongozi hao wanne wa ODM ni sababu kuu ya kutofanyika kwa maandamano katika maeneo hayo siku ya Alhamisi (Agosti 8,2024). Wakazi hawakuona haja ya kuandamana ilhali sasa wanahisi kuwa ndani ya serikali,” Profesa Kanyinga aliambia Taifa Leo jana.

“Sasa Rais Ruto ameonekana kupata afueni baada ya kupungua kwa presha za Gen Z kiasi kwamba sasa anaweza kufanya ziara nje ya nchi. Baada ya Rwanda, huenda akazuru mataifa mengine hata nje ya Afrika alivyofanya kabla ya ujio wa maandamano hayo,” akaongeza msomi huyo ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Ruto amkinga Rigathi

Rais Ruto pia amezuru Rwanda siku moja baada ya kukutana na kundi la wabunge kutoka Mlima Kenya, ambapo inasemekana alifaulu kuwashawishi kuondoa mipango ya kuwasilisha hoja ya kumtimua Naibu wake Rigathi Gachagua.

Wakati wa mkutano huo uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi, wabunge hao waliahidi kukomesha vita vya kisiasa kati yao na Bw Gachagua na kushirikiana naye kufanikisha ajenda za serikali ya Rais Ruto.