Afya na Jamii

Mbinu zinazosaidia kurekebisha mpangilio wa meno

Na WANGU KANURI August 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

WATU mbalimbali hujipata wakikabiliwa na changamoto tofauti za meno, baadhi wakitaka kufunga mwanya waliozaliwa nao, wengine wakitatizwa na hali ya meno kumea kwa hali isiyokuwa ya kawaida.

Baadhi yao huamua kutafuta ushauri na usaidizi kutoka kwa madaktari wa meno, huku teknolojia nayo ikiendelea kuvumbuliwa na kuhakikisha kuwa hali ya meno yao haiwanyimi tabasamu.

Peris Mwangi anasimulia kuwa aliamua kuweka vifaa vya kubana na kulainisha meno almaarufu braces ili kuziba mwanya uliokuwepo kwenye meno yake ya juu.

Kwa muda wa matibabu, Bi Mwangi anasema kuwa mwanya huo hatimaye ulizibika. Alipotolewa vifaa vile, alivalishwa kifaa cha chuma kinachowekwa juu ya meno yako almaarufu retainer ili meno yake yasalie pale pale.

“Miaka iliposonga, kifaa kile kilivunjika na mwanya uliokuwa katikati ya meno yangu ukarudi tena,” anasema japo hajarudi kurekebisha tena.
Kama Bi Mwangi, Dkt Naphtali Macharia, mtaalam wa meno katika The Dental Spa, anasema kuwa watu wanaohitaji vifaa hivi huwa na meno ambayo hayajajipanga vizuri kwenye ufizi.

Kutojipanga huku hutokea kwa njia mbalimbali kama; meno hayakutoshea kwenye ufizi, kuwa na meno mengi, ufizi kuwa mkubwa zaidi ya meno na kuwacha mianya, meno ya juu na ya chini hayashikani ukifunga ufizi na meno ya juu hayashikani na ya chini ukifunga ufizi wako.

Hata hivyo, wengi wa wagonjwa wake huwa na meno yasiyotoshea kwenye ufizi kwa sababu ya meno hayo kuwa makubwa ukilinganisha na ukubwa wa ufizi.


Kifaa kinachofahamika kama retainer ambacho hutumiwa baada ya braces kutolewa ili kusaidia udumisha mpangilio wa meno ikiwa mwanya umefungwa. PICHA| BONFACE BOGITA

Ili kurekebisha hali hiyo, Dkt Macharia anasema kuwa wakati mwingine yeye hung’oa meno mengine ili kutengeneza mwanya au kupunguza saizi ya meno.

“Vifaa hivi vya kubana meno huhakikisha kuwa meno yako yana mpangilio maalum kwa kutumia chuma ndogo zinazowekwa kwenye sehemu ya juu ya meno (brackets), na waya inayoshikanisha chuma hizo,” Dkt Macharia anafafanua.

Japo matatizo haya ya meno yanaweza kutibiwa kwa kutumia vifaa vya kubana meno, ni vyema kutochelewa kurekebisha mpangilio wa meno yako.

Dkt Macharia anashauri kuwa mtoto huwekwa vifaa hivyo vya kubana meno baada ya kuota meno yake yote ya kudumu.

“Kutoka umri wa kubaleghe hadi kabla miaka 30, ni vizuri kurekebisha meno yako kwa sababu wakati huo meno husonga na kujipanga haraka ikilinganishwa na baada ya miaka 30 na zaidi,” anasema.

Baada ya kuwekwa braces

Hata hivyo, baada ya kuwekwa vifaa hivi, huenda mgonjwa akahisi usumbufu kwenye meno usio na maumivu.

Hali hii huchangiwa na meno kuletwa pamoja. Pia, Dkt Macharia anasema kuwa mgonjwa huyu hataweza kula vyakula kama bisi (popcorn), nyama ya mfupa, njugu, ili usivunje chuma ile iliyowekwa kwenye meno.

“Ukivunja chuma hiyo basi unachelewesha kipindi chako cha kupata nafuu na kutovaa kifaa hicho cha kubana meno,” anasema.

Isitoshe, mgonjwa huyu anapaswa kurudi hospitalini baada ya wiki nne au tano ili waya iliyowekwa ibadilishwe.

Dkt Macharia anaeleza kuwa mwanzoni waya hii huwa nyembamba lakini baada ya meno kuanza kusonga, mgonjwa huvalishwa waya nene ili kusukuma meno zaidi na zaidi.

Huku kanuni ya kupiga mswaki ikiwa mara mbili kwa siku kwa dakika mbili, Dkt Macharia anafafanua kuwa wagonjwa wanaovalia vifaa vya kubana meno wanapaswa kupiga mswaki mara mbili kwa siku kwa dakika tano.

“Hii ni kwa sababu chuma hizo kwenye sehemu ya meno hushikilia uchafu na mabaki ya chakula. Pia, unaweza ukatumia kifaa kinachorushia meno maji (water flosser) au brashi ndogo inayotumika kuosha katikati ya meno pale ambapo mswaki wa kawaida haufikii (interdental brush),” anaelezea.

Muda wa kuvaa braces

Unapaswa kuvaa kifaa hiki cha kubana meno kwa muda wa mwaka mmoja au hata miaka miwili na nusu kulingana na urekebisho uliofaa wa meno yako.

Dkt Macharia anasema kuwa waya inayopita kwenye chuma hutumia nguvu kidogo kusongesha meno bila mgonjwa kuhisi uchungu. “Pale jino hilo huelekea ili lijipange; tishu ya mfupa huo huvunjwa vunjwa ili kupatia jino hilo nafasi (bone resorption),” anasema.

Baada ya kutoa braces

Baada ya kutoa kifaa hicho kilichokusaidia kubana na kupanga meno, Dkt Macharia anashauri kuwa mgonjwa huyo anapaswa kuvaa kifaa cha plastiki au chuma kinachoketi juu ya meno yako almaarufu (retainer).

“Kifaa hiki husaidia kuhakikisha kuwa meno yamesalia pale yalipojipangia bila kusonga. Hii ni kwa sababu mfupa huu mpya uliopangiwa meno huchukua muda wa angalau miaka 2-3 au hata milele, kuwa imara.”

Hata hivyo, mgonjwa huyu anaweza kupiga mswaki mara mbili kwa siku kwa dakika mbili lakini ahakikishe kuwa haathiri kule kifaa hiki kiliwekwa.

Dkt Macharia anasema kuwa kifaa hiki huwekwa kwa muda mrefu au milele kwenye meno ya chini lakini cha meno ya juu mgonjwa anaweza akakitoa. Cha muhimu ni kuhakikisha umedumisha usafi.

“Kioshe kwa kutumia maji na kitambaa na unapokitoa hakikisha kuwa mikono yako ni safi,” anasema.