Wandayi: Kama kitu nitapigana vikali kupunguza ni bei ya stima
WAZIRI mpya wa Kawi na Bidhaa za Petroli Opiyo Wandayi ametoa hakikisho kuwa kupunguzwa kwa bei ya umeme ni miongoni mwa masuala atayoyapa kipaumbele anapoendesha majukumu ya wizara hiyo.
Bw Wandayi Jumatano, Agosti 14, 2024, alisema kuwa Wakenya wengi hawawezi wakamudu bei ya huduma hiyo wakati huu ambapo gharama haijashuka.
Akiingia afisini rasmi baada ya kuteuliwa rasmi na Rais William Ruto kushikilia wadhifa huo, Bw Wandayi alisema anatambua mchango mkubwa wa Wizara ya Kawi katika kuendesha ukuaji wa uchumi wa Kenya.
Mbunge huyo wa zamani wa Ugunja, ambaye alipokezwa afisi rasmi na aliyekuwa Waziri katika Wizara hiyo Davis Chirchir ambaye sasa ni Waziri wa Uchukuzi na Barabara, alisema kuwa yu tayari kushirikiana na wadau katika kufanikisha mageuzi katika sekta.
Ili kupunguza bei ya umeme, Bw Wandayi aliahidi kufanya mazungumzo na kampuni ya kusambaza umeme nchini (KPLC) kuhusu namna ya kupunguza hasara ya kupotea kwa nguvu za umeme kutoka kima cha asilimia 23 hadi angalau asilimia 15.
“Tukifanya hivyo, ambayo naamini tutafanya hivi karibuni, gharama ya umeme itashuka. Hii ni licha ya ukweli kwamba bei ya umeme na petroli huchangiwa na mambo mbalimbali,” waziri akaeleza.
Bw Wandayi pia alisema anaingia afisini huku akikumbatia njia mpya za kuendesha shughuli ambayo itahusisha ushirikiano wa karibu na wafanyakazi wa kampuni za kawi, wadau na wateja wa umeme na bidhaa za petroli.
Vile vile, Waziri alisema kuwa anakuendeleza uwazi na uwajibikaji katika kuendesha mchakato wa kupunguza gharama ya umeme na bidhaa za petroli.
“Tunataka kuendeleza utamaduni na moyo wa uwazi katika uendeshaji wa masuala ya wizara hii ya kawi. Tunataka kugeuza sura ya wizara hii ili iwe kitovu cha huduma kwa wananchi,” Bw Wandayi akaongeza.
Waziri alikariri haja ya ushirikishwaji wa wananchi katika utekelezaji wa majukumu ya wizara ya kawi.
“Hii ndio njia ya kipekee ya kurejesha imani ya wananchi kwa wizara hii,” Bw Wandayi akasema.
“Isitoshe, nitaandaa majukwaa kwa kuwezesha maafisa wa Wizara hii kushauria na wateja wetu mara mbili kila wiki. Majukwaa kama haya yatatuwezesha kupata hisia na majibu kutoka kwa umma kuhusu utendakazi wetu kama wizara,” akaongeza akieleza kuwa hiyo ndio njia bora ya kuwawezesha Wakenya kujua yale yanayoendelea katika Wizara ya Kawi.
Kwa upande wake, Bw Chirchir aliahidi kuelekea kumsaidia na kumwelekeza Bw Wandayi anapoendelea kujifahamisha na masuala mbalimbali kuhusu wizara hiyo.
“Wizara hii imekuwa ikilaumiwa mara kadhaa stima inapopotea katika maeneo mbalimbali. Nitaendelea kumsaidia ndugu yangu Wandayi kukabiliana na changamoto kama hizi zinapotokea,” akasema.