Habari za Kitaifa

Hapa mnatumaliza, walia wakulima wa ndengu huku Seneta mwenye mswada akijitetea


SENETA Enoch Wambua aliyedhamini Msawada wa Pojo 2022, amekana ripoti katika vyombo vya habari kwamba wakulima wa pojo (ndengu) watahitajika kupata leseni ya kushiriki kilimo cha zao hilo la sivyo watozwe faini ya Sh1 milioni au kifungo cha miaka miwili gerezani.

Hii ni ikiwa Mswada wa Pojo wa 2022 utapitishwa kuwa sheria.

Kwenye taarifa aliyoitoa Alhamisi, Bw Wambua alifafanua kuwa ni watu wenye nia ya kuendesha biashara na utengenezaji bidhaa kutokana na zao hilo wanaohitajika kupata leseni, kulingana na mswada huo.

“Hitaji la kupata leseni kwa wafanyabiashara na waongezeaji thamani kwa zao la pojo limeelezwa wazi katika Sehemu ya 9 (1) ya mswada huo,” akaeleza.

Seneta Wambua akaongeza: “Usajili wa wakulima wa pojo wenye mashamba madogo na yale ya ukubwa wa kati unalenga kuisaidia serikali kuelewa vyema kilimo hicho na kuendeleza sekta hiyo. Aidha, data kutokana na usajili utaiwezesha serikali kufanikisha mikakati ya kuboresha kilimo hicho ili zao hilo linunuliwe kwa wingi katika masoko ya humu nchini na kimataifa.”

Bw Wambua alisema hayo huku wakulima kutoka kaunti za Embu na Kirinyaga ambao walihofia kuwa mswada huo huenda ukawaathiri wakitoa maoni yao.

“Huo mswada hauwasaidii wakulima na tunaukataa kabisa,” akasema mkulima wa pojo Embu, Bi Miriam Wanjeru.

Wakulima wamesema mswada huo ni hatari kwa sababu sasa watakuwa wakilipa leseni jambo ambalo hawalifanyi sasa.

Wale ambao wataathirika sana ni wale ambao wanatoka kaunti kame ambako pojo imekuwa ikikuzwa kwenye mashamba makubwa na ni kitega uchumi.

“Sisi tunategemea kilimo cha pojo hasa wakati wa ukame. Itakuwa vigumu sana kwetu kupanda pojo iwapo ni lazima tulipie leseni,” akasema Bi Wanjeru kutoka kijiji cha Kiywe Mbeere Kaskazini.

Wakulima hao walilalamika kuwa hawataweza kulipia leseni kukuza pojo iwapo mswada huo utapitishwa.

“Kile ambacho kinafanyika ni kama kuwatoza wakulima ushuru ilhali wanapambana kulima pojo kutokana na gharama ya juu ya pembejeo za kilimo,” akasema Bw Njoka Njagi ambaye pia ni mkulima.

Mkulima huyo alisisitiza kuwa yaliyomo kwenye mswada huo ni hatari kwa kilimo chao na hayafai kuvumiliwa au kukubaliwa popote.

Bi Rose Njagi kutoka Kaunti ya Kirinyaga, naye alisema hatua ya kudhibiti kilimo cha pojo haifai na wakulima wanastahili kupewa uhuru wa kuendeleza kilimo chao bila ushuru.

“Inakuaje wakulima watatakiwa kulipia leseni kukuza pojo kwenye mashamba ambayo wao ndio wanamiliki?” akauliza Bi Njagi.

“Iwapo mswada huo utapita, basi wakulima wengi watakiasi kilimo cha pojo kwa sababu hawatamudu pesa za kulipia leseni na hilo litachangia ukosefu wa chakula cha kutosha nchini,” akasema Bi Njagi.

Hata hivyo, kulingana na Seneta huyo wa Kitui Mswada wa pojo hauhitaji wakulima kupata leseni kabla ya kushiriki kilimo cha zao hilo.