Habari za Kitaifa

Nilijaribu kumshawishi mamangu kwa zawadi asirejee msituni Shakahola ila alikataa -Shahidi

Na BRIAN OCHARO August 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SHAHIDI mmoja ameambia mahakama ya Mombasa kwamba alijaribu kumwokoa mamake kutokana na mahubiri makali ya pasta Paul Mackenzie lakini akaishia kupotelea msituni baada ya kukataa kusikiliza ushauri wake.

Shahidi huyo alimweleza Hakimu Mkuu Alex Ithuku kwamba majaribio yake mengi ya kumuokoa mamake kutoka kwa Mackenzie na mafundisho yake mabaya yaliangukia patupu.

Hii ilikuwa Februari 2023, miezi miwili tu kabla ya makaburi ya halaiki kufunuliwa katika msitu wa Shakahola, ambapo wafuasi wa Mackenzie walikuwa wamehamia.

Mama huyo ambaye alihamia msituni pamoja na waumini wengine wa kanisa la Good News International (GNI) mnamo 2020 alikuwa amerejea nyumbani kwao Malindi mnamo Februari 2023.

“Alionekana dhaifu na kueleza kuwa hakukuwa na mvua na alikuwa akikabiliwa na uhaba wa chakula. Alikaa nyumbani kwa takriban wiki moja ambapo mimi na ndugu zangu tulijaribu kumsihi asirudi huko,” alisema shahidi huyo huku akitokwa na machozi.

Shahidi huyo ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 16, alisema kaka yake mkubwa hata alimnunulia mama yao zawadi, simu ya mkononi, katika jitihada za kumshawishi asirudi msituni.

Hii, hata hivyo, haikumshawishi mama yao. Asubuhi moja, akiwa anajiandaa kwenda shule, aligundua kuwa mama yake pia alikuwa ameamka na kutayarisha nguo zake.

“Nilipokuwa nikielekea shuleni asubuhi hiyo, nilimwona pia akitembea kuelekea katika kituo cha kuabiria magari cha Malindi. Hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya mwisho kumuona,” alisema shahidi.

Shahidi huyo, akiongozwa na timu ya upande mashtaka inayojumuisha Jami Yamina, Victor Owiti, Victor Simbi, Yassir Mohamed, Alex Gituma, Betty Rubia, na Hillary Isiaho, alisema alipouliza, mamake alimwambia kuwa anarejea Shakahola.

Baada ya kuondoka, alizungumza naye mara kadhaa lakini hakuweza kumpata mwishoni mwa Februari 2023, kwa kuwa simu yake haikuwa ikipatikana.

“Siku moja nikiwa naelekea nyumbani kutoka shuleni, mshiriki wa zamani wa kanisa la GNI, alinijulisha kwamba alikuwa amepokea habari za watu kufariki huko Shakahola na kwamba maiti nne zililetwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Malindi,” alisema.

Baada ya kupata taarifa hizo za kushtua, alienda katika Kituo cha Polisi cha Malindi, ambako aliandikisha taarifa kwamba mama yake ni miongoni mwa waliohamia Shakahola.

“Baadaye nilichukua simu na kumpigia Mackenzie kumuuliza mama yangu alipo na hali yake lakini simu yake ilikuwa haipatikani,” alisema.

Asubuhi iliyofuata, walikwenda katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Malindi kuangalia miili ya wanaume wanne na mwanamke mmoja waliofariki huko Shakahola na kuletwa katika kituo hicho.

Alimchunguza yule mwanamke na kuona si mama yake na baadaye kwa mara nyingine akampigia simu Mackenzie.

“Alipopokea simu yangu, aliniambia kwamba hakuweza kujua alipo mamangu wakati huo kwa sababu watu walikuwa wametawanyika sehemu tofauti za msitu,” alisema.

Mtoto huyo alizaliwa na kukulia katika familia ya Kiislamu ambapo wazazi wake na ndugu zake walikuwa Waislamu.

Walihudhuria Madrasa (darasa za Kiislamu) huko Malindi. Hata hivyo, siku moja aliugua baada ya kifo cha baba yao, hivyo mama yao aliwaagiza wasihudhurie masomo ya Madrasa badala yake waandamane naye hadi kanisa la Mackenzie eneo la Furunzi Malindi.

“Ningependa kuthibitisha kwamba mimi na dada yangu tulikwenda pamoja na mama yetu katika kanisa hilo siku ya juma, na nikiwa huko, mchungaji ambaye nilimfahamu baadaye aliitwa Paul Mackenzie aliniombea na nikapona,” aliambia mahakama.

Kuanzia wakati huo na kuendelea, wawili hao waliacha kuhudhuria madarasa na kujiunga na kanisa la Mackenzie kwa ibada za Jumapili. Kisha wakaandikishwa katika masomo ya funzo la Biblia, kabla ya kuzuiliwa kuhudhuria elimu rasmi.

Mnamo 2017, shahidi huyo alikuwa miongoni mwa watoto saba waliokamatwa pamoja na Mackenzie kwa kukataa kuhudhuria shule rasmi. Hata hivyo, waliachiliwa na kuwa mashahidi wa serikali dhidi ya Mackenzie.

Mackenzie na timu yake wamekanusha mashtaka 238 ya kuua bila kukusudia, wakidai kuwa vifo vya Shakahola havihusiani na uhuru wa kuabudu na kukusanyika waliyokuwa wakiendesha msituni.

Kupitia wakili wao, Lawrence Obonyo, wamesisitiza kwamba mafundisho na imani yao inatokana na Biblia.Kesi hiyo itasikilizwa Septemba 9.