Habari za Kaunti

Naibu Gavana wa Uasin Gishu Mhandisi John Barorot ajiuzulu ghafla


PENGO la uongozi limetokea katika serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu baada ya Naibu Gavana John Barorot kujiuzulu ghafla.

Bw Barorot alitoa tangazo hilo Jumatatu, Agosti 19, 2024 wakati wa mkutano wa maafisa wa ngazi za juu katika kaunti hiyo ulioongozwa na Gavana Jonathan Bii katika mkahawa mmoja jijini Eldoret.

Naibu huyo wa Gavana amejiuzulu siku chache baada ya kufutilia mbali uvumi kwamba anapania kujiondoa.

Hata hivyo, uvumi huo ulionekana kupata mashiko Jumatano wiki iliyopita alipokwepa kuhudhuria sherehe ya kupandishwa hadhi ya manisipaa ya mji wa Eldoret kuwa jiji.

Licha ya kupuuzilia mbali uvumi kuhusu kujiuzulu kwake, Bw Barorot hakueleza ni kwa nini alifeli kuhudhuria hafla hiyo iliyoongozwa na Rais William Ruto katika uwanja wa Eldoret Sports Club.

Dkt Ruto alikuwa ameandamana na naibu wake, Rigathi Gachagua.

Duru zinasema kuwa uhusiano kati ya Gavana Bii na Mhandisi Barorot haujakuwa mzuri katika siku za hivi karibuni.

Inakisiwa kuwa hiyo ndio sababu naibu huyo wa Gavana amekuwa akijitenga na shughuli kuu za Kaunti ya Uasin Gishu, haswa maandalizi ya sherehe ya kuipandisha hadhi Eldoret kuwa jiji la tano nchini Kenya.

Kulingana na Sehemu ya 33 ya Sheria ya Serikali za Kaunti, Gavana anapaswa kuteua Naibu Gavana mpya siku 14 baada ya nafasi hiyo kusalia wazi, kwa njia zinatombuliwa kisheria.

Njia hizo ni; kifo, kuondolewa afisini, kushindwa kutekeleza majukumu ya afisi au kujiuzulu.