Habari za Kitaifa

Kanja pazuri kwa IG kamati ya Bunge ikiidhinisha arithi Koome

Na BENSON MATHEKA August 20th, 2024 1 min read

KAMATI ya pamoja ya bunge imemuidhinisha Douglas Kanja kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) kumrithi Japhet Koome aliyejiuzulu.

Kamati ilimhoji Bw Kanja wiki jana na Seneti inajadili ripoti ya kamati hiyo.

Bw Kanja, 60, aliahidi wabunge na maseneta waliokuwa wakimhoji kubaini ufaafu wake kwa wajibu huo, kwamba atapambana vikali na zimwi la ufisadi kwenye polisi.

Alisema atafanya hivyo kwa kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika udumishaji usalama kwa kuamuru maafisa wote wavalie beji zenye majina yao wakiwa kazini.

“Aidha, nitapambana na polisi wanaoshiriki mgongano wa kimasilahi wakiwa kazini.

“Polisi watalazimika kuamua kufuata mkondo mmoja,” akasema Bw Kanja ambaye amehitimu kwa Shahada ya Digrii katika Masuala ya Biashara.

“Nilipohudumu kama Naibu Inspekta Jenerali, niligundua kuwa baadhi ya maafisa wa polisi ndio wamiliki wa matatu zinazovunja sheria au mabaa yanauza pombe haramu. Niliwaambia chaguo ni kufuata mkondo mmoja, kuacha kazi ya polisi na kuendesha biashara ya matatu au kuacha biashara ya matatu na kujishughulisha na kazi katika NPS,” Bw Kanja, ambaye amehudumu kama afisa wa polisi kwa miaka 39, akaambia Kamati ya Pamoja ya Bunge la Kitaifa na Seneti iliyokuwa ikimpiga msasa Alhamisi katika majengo ya bunge.

Atateuliwa rasmi ripoti ya kamati hiyo ikiidhinisha na mabunge yote mawili.