Habari za Kitaifa

Mikakati ya serikali kudhibiti maambukizi ya Mpox

Na EVANS JAOLA August 21st, 2024 1 min read

SERIKALI ya Kenya imeimarisha doria katika mpaka wake na Uganda ili kuzuia maambukizi zaidi ya ugonjwa wa homa ya nyani (Monkeypox).

Idara ya Afya katika Kaunti ya Trans Nzoia imechukua tahadhari kuhusu mlipuko wa ugonjwa huo kutoka nchi jirani ya Uganda, huku wahudumu wa afya wakishika doria kwenye mpaka wa Suam.

Afisa anayedhibiti mlipuko wa magonjwa katika Kaunti hiyo, Bw Brian Ateka, alibainisha kuwa wizara ya afya imeanzisha kituo cha uchunguzi wa mashirika mbalimbali kwenye mpaka wa Suam ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo nchini.

“Timu mbalimbali ziko humo tayari kushughulikia dharura yoyote. Maafisa wetu wa uchunguzi wa magonjwa pia wako katika hali ya tahadhari hasa kuangalia watu wanaoingia ndani ya nchi na wanaotoka,” Bw Ateka aliambia Taifa Dijitali.

Watu wote wanaoingia au kutoka nchini, wanachunguzwa kama itifaki ya kimsingi ya afya ili kuzuia maambukizi yoyote ya ugonjwa huo.

“Wale wote wanaopita mpakani wanapaswa kuchunguzwa kabla ya kuingia Kenya. Hii ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kwamba kaunti na eneo letu liko salama,” aliongeza.

Kamati ya Kukabiliana na Dharura katika Kaunti hiyo iliyoanzishwa wakati wa janga la corona, imenaza kutekeleza jukumu lake kama sehemu ya hatua za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo nchini.